Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amewatoa hofu wana Singida na watanzania wote kuwa
kuelekea kipindi cha mvua barabara kuu zote za kuingia na kutoka Mkoani Singida
zinapitika vizuri.
Dkt Nchimbi ameyasema
hayo mara baada ya kukagua ukarabati wa barabara ya Malendi Wilayani Iramba
ambapo ameridhishwa na ubora wa kazi hiyo huku akimtaka Mkandarasi wa barabara
hiyo kuongea muda wa kazi ili kukamilisha matengenezo makubwa kabla ya mvua
kubwa kuanza.
Amesema barabara kuu za
Kuingia na kutoka Singida ni kiunganishi cha mikoa katika kila upande pamoja na
kuiunganisha mikoa hiyo na nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na Kongo ambazo
hutumia barabara hizo.
Dkt Nchimbi amemtaka
mkandarasi Medics Technique Group of Company kuichukulia kwa uzito na thamani
ya kimataifa barabara ya Malendi kwa kuwa kutokamilika kwa muda kutawaadhiri
watanzania wengi na nchi za jirani kushindwa kusafirisha bidhaa zao kwa wakati.
“Thamani ya barabara
hii sio ya ki mkoa, hapa pakiwa na shida watakaoumia sio wana Iramba au Singida
pekee, kuna magari yanasafirisha bidhaa kutoka bandarini Dar es Salaam kuelekea
nchi za jirani watapata shida pia, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha hapa
panapitika kwa usalama”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa
kutokana na matarajio ya Mkoa wa Singida kupata mvua za wastani na juu ya
wastani mkandarasi huyo aongeze masaa mawili kila siku ili kazi hiyo iishe
mapema na ifikapo mwezi Disemba magari yaweze kupita juu ya hiyo barabara.
Dkt Nchimbi amemtaka
mkandarasi huyo kutengeza njia ya mchepuo yenye viwango vya juu ili barabara
hiyi ipitike wakati wowote na katika hali yoyote ile.
Aidha amezitaka
halmashauri kujiandaa kupokea mvua kwa kukagua mabwawa kama yanaweza kupokea
maji ya mvua vizuri pamoja na mifereji inayopitisha maji isafishwe mapema ili
mvua hizo zisilete madhara bali zisaidie kuifanya Singida kuwa ya Kijani na
yenye maji ya kutosha.
Amewaasa wananchi
kuandaa mashamba kwa ajili ya kilimo ili wasipishane na kipindi cha kulima,
kupanda au palizi bila kusahau kurekebisha makazi yao ili yawe imara kwa kuhimili
mvua za aina yoyote.
Kwa upande wake Meneja
wa TANROADS Mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo amesema mradi wa Malendi
unahusisha matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita mbili kwa upande wa
Singida na mita 500 kwa upande wa Mkoa wa Tabora huku ukigharimu shilingi
bilioni tatu.
Mhandisi Kapongo
amesema Mkandarasi Medics Technique Group of Company anatarajiwa kukamilisha
kazi zote mwezi Machi mwakani kwa kujenga madaraja mawili, makaravati mawili na
barabara hiyo kwa kiwango cha lami ijapokua hadi kufikia Disemba barabara hiyo
itapitika bila ya lami.
Ameongeza kuwa ana
imani kuwa mkandarasi huyo mzawa atakamilisha kazi hiyo kwa uboa unaotakiwa kutokana
na ujuzi na vifaa alivyonavyo huku akieleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo
kutafanya barabara zote kuu kuwa katika kiwango cha lami yenye ubora zaidi.
Naye Diwani wa Kata
ya Mgongo Mkumbo Wilson ameishukuru serikali kwa kufanya marekebisho katika
barabara hiyo ya Malendi kwakuwa imekuwa ni eneo lenye matatizo hasa kipindi
cha mvua nyingi.
Wilson amesema
kipindi cha mvua hasa miaka miwili iliyopita maji yalikuwa yanajaa na kufunika
barabara hiyo hivyo kuhatarisha maisha ya wasafiri na wakazi wa Malendi.
Ameongeza kuwa uharibifu
wa mazingira katika mashamba yaliyo jirani na barabara hiyo yameongeza tatizo
la kujaa maji eneo hilo kwakuwa mvua zikinyesha maji yanashindwa kuzuiwa
mashambani na kujaa barabarani hivyo wataongeza bidii katika kuelimisha jamii
juu ya utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment