WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt Steven
Kebwe na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kwenda katika kijiji cha
Maseyu kufuatilia utendaji wa kampuni ya Zhong Fenq kama inafuata
sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumamosi, Septemba 2, 2017), wakati akizungumza na viongozi na
watumishi wa kiwanda cha Philp Morris kinachotengeneza sigara aina ya
Marlboro akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya viwanda mkoani
Morogoro.
Agizo hilo limefuatia malalamiko ya
mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mheshimiwa Omary Mgumba kuwa
wawekezaji hao kutoka China wanaendesha shughuli za uchimbaji wa mabo
katika kijiji cha Maseyu wilayani Morogoro bila ya kuwa na kibali.
Mheshimiwa mgumba amesema tangu mwaka
2011 wawekezaji hao wameendesha shughuli zao bila kulipa kodi za
Serikali na tozo za Halmashauri, hivyo kuikosesha Serikali mapato.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kijiji
cha Maseyu kuna Wachina wa kampini ya Zhong Fenq wanachimba mabo na
hawana kibali na hakuna kodi yoyote wanayolipa Serikalini tangu mwaka
2010 walipoanza uzalishaji.”
Mbunge huyo ambaye machimbo hayo yako
jimboni kwake aliongeza kwamba licha ya uongozi wa mkoa kwenda katika
eneo hilo na kuizuia kampuni kuendelea na uchimbaji hadi itakapopata
vibali walikaidi na kuendelea na shughuli.
Waziri Mkuu amesema hakuna muwekezaji
anayeruhusiwa kufanya kazi bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu za
nchi. Hivyo ameagiza kesho Mkuu wa Mkoa afuatilie Wachina hao na kuona
namna gani wamezingatia sheria za nchi.
Amesema iwapo watabaini kwamba
wawekezaji hao hawajafuata sheria, kanuni na taratibu hatua zichukuliwe
dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika eneo hilo chini ya ulinzi
na kuwasiliana na ubalozi wa China Nchini.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kutoa wito kwa watu wote wenye nia ya kutaka kuwekeza katika miradi
mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na
taratibu za uwekezaji.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amesema ni faraja kuona kiwanda cha Philp Morris kikiwa kimekamilika
tayari kwa kuanza uzalishaji wa sigara aina ya Marlboro hivyo kuwezesha
wakulima wa tumbaku nchini kuwa na soko la uhakika.
Amesema miaka ya nyuma uzalishaji wa
tumbaku ulipungua nchini kutokana na wakulima kukata taama baada ya
kukosa soko la uhakika pamoja na kuchoshwa na ubadhilifu wa mali za
ushirika uliokuwa ukifanywa na viongozi wa vyama vya ushirika wa
tumbaku.
Pia Waziri Mkuu alitembelea ujenzi wa
kiwanda cha sukari kilichopo katika Gereza la Mbigiri wilayani Kilosa na
kukagua shamba la miwa lenye ukubwa wa hekta 4,800 ambapo hekta 320
zimelimwa na kati yake hekta 125 tayari zimepandwa miwa na imeshaota.
Kiwanda hicho kinajengwa kwa
ushirikiano wa Jeshi la Magereza na mifuko ya hifadhi ya Jamii ya NSSF
na PPF kupitia mradi wa Mkulazi ambao unatarajia kuzalisha tani 250,000
za sukari kwa mwaka kati yake tani 50,000 zitazalishwa katika kiwanda
cha Mbigiri na tani 200,000 katika kiwanda cha Ngerengere.
Amesema uwepo wa viwanda nchini
utawezesha watanzania kulima kilimo chenye tija kwa kuwa watauza mazao
yao viwandani na mmoja atashiriki kulima zao ambalo ataliuza katika
kiwanda cha jirani.
No comments:
Post a Comment