Na Beatrice Lyimo – MAELEZO- Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Zainab Chaula amewaasa
watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu kwa
maendeleo ya taifa.
Dkt. Chaula ameyasema hayo wakati
alipokuwa akifunga mafunzo ya siku nane ya Mfumo wa Kielektroniki wa
Kuandaa Mipango, Bajeti na Ripoti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa
(PlanRep) iliyoboreshwa leo mjini Dodoma.
“Nina imani kila mtu kwa nafasi
aliyonayo anatakiwa kutimiza wajibu wake kufanya kazi kwa weledi na
uwajibikaji kulingana na ujuzi alionao” ameseza Dkt. Chaula.
Aidha Dkt. Chaula ametoa wito kwa
watumishi wa Serikali kuwajibika kwa kufuata Sera ya Ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) Chama kilichopo madarakani ambacho kina mkataba na
wananchi wa kuwatumikia.
“Watendaji wa Serikali hawapaswi
kuwa na Chama, wanapaswa kufuata ilani ya Chama tawala kilichopo
madarakani na utekelezaji wake ni mkataba kati ya Chama na Wananchi”
amesema Dkt. Chaula.
Hata hivyo, Dkt. Chaula
ameupongeza Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) kwa mafunzo hayo
kwani Mfumo wa kielektroniki wa kuandaa Mipango, Bajeti na Ripoti za
Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep) umekuwa mkombozi wa changamoto
zilizokuwa awali katika uaandaaji wa Mipango na Bajeti za Serikali.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa
Mifumo ya TEHAMA kutoka Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) Desderi
Wengaa ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ushirikiano katika
kufanikisha mradi.
“Mradi wa Uimarishaji Sekta za
Umma (PS3) umejipanga katika kuzisaidia Halmashauri zote nchi nzima
ambapo timu za wawezeshaji zitakwenda kila Halmashauri kuona utekelezaji
wa mafunzo kwa wale ambao wamepata mafunzo haya” alisema Bw. Wengaa.
Aidha, Bw. Wengaa ameongeza kuwa
katika kipindi cha uandaaji wa bajeti za Serikali yaani mwezi Octoba
timu za wawezeshaji zitakwenda kila Halmashauri kwa miongozo mbalimbali
ya mfumo huo.
Naye mwakilishi wa washiriki wa
mafunzo hayo Bw. Bartholome Temba kwa niaba ya washiriki wenzake
ameushukuru uongozi wa Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) kwa
mafunzo waliopatiwa na kuahidi kutekeleza vyema mfumo huo kwa maendeleo
ya Taifa.
No comments:
Post a Comment