Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud
akieleza mafanikio ya Jumuiya tokea ilipoasisiwa mwaka jana katika
mkutano uliofanyika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na
Uchumi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja Ali Juma Ali
akiwaeleza wananchama wa Jumuiya hiyo mikakati na mipango ya kuiendeleza
ili kufikia malengo yake katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Baraza la
Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Makamu wa Pili wa Rais Balozi
Seif Ali Iddi akifungua mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa
Kaskazini Unguja katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani
Kikwajuni.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja wakifuatilia mkutano huo
uliofanyika Baraza l a Wawakilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Makamu wa pili wa Rais Balozi
Seif Ali Iddi akiagana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa
Kaskazini Unguja Ali Juma Ali baada ya mkutano wa Jumuiya hiyo
uliofanyika Ukumbi wa Baraza la wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Picha na Makame Mshenga.
………………………………………………………………………….
Na Miza Kona, MAELEZO
MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi
Seif Ali Iddi, ameitaka Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja
kuzidisha mshikamano ili kuweza kubadilika kielimu na kuleta maendeleo
mazuri mkoani humo.
Balozi Seif ameyasema hayo katika
ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar
katika mkutano wa Jumuiya hiyo.
Alisema vijana wengi wa mkoa huo wanakosa kuingia katika ushindani wa soko la ajira kutokana na kukosa sifa zinazohitajika.
Balozi Seif alisema jumuiya
inaweza kuleta mafanikio makubwa kwa kushirikana pamoja na kuzidisha
mshikamano katika dhamira ya kuibadilisha jamii ya mkoa huo kielimu.
Alifahamisha kuwa elimu ndio
silaha pekee inayoweza kuwakomboa vijana na kuwawezesha kukubalika
katika ajira mbalimbali na hivyo kuondokana na umasikini.
“Ni wakati sasa wa kubadilika kwa
kuwekeza katika elimu ya watoto wetu ili kuwainua vijana na kuwawezesha
kuhimili ushindani kwa kuwa na sifa zitakazoweza kuajiriwa au
kujiajiri,” alifahamisha Balozi Seif.
Alieleza vijana wengi wa mkoa huo
hawana mwamko wa kusoma, jambo linachangia mkoa wa Kaskazini kuwa nyuma
kielimu na kimaendeleo ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.
Amehimiza kuwepo ushirikiano wa
pamoja baina ya viongozi na wana jumuiya katika kuishajiisha jamii ili
iweze kubadilika kiuchumi na kuacha kuingiza itikadi za siasa katika
suala la kuleta maendeleo.
Balozi Seif alisema jumuiya ina nia ya kuimarisha umoja na kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais
amewasisitiza viongozi wa majimbo na serikali katika mkoa huo kudumisha
ushirikiano na kuwasaidia vijana wasio na uwezo wa kujikimu kwa kuwapa
msukumo wa kimaendeleo pamoja na kuishajiisha jamii kujiunga jumuiya
hiyo.
Jumuiya Maendeleo ya Mkoa wa
Kaskazini Unguja (NUDO), imeasisiwa mwezi Aprili 2016, na sasa ina zaidi
ya wanachama zaidi ya 1000.
Lengo la kuanzishwa kwake ni
kuendeleza, kuwezesha na kuijengea uwezo jamii ya mkoa huo katika kuinua
ustawi wake kiuchumi, kijamii na mazingira.
No comments:
Post a Comment