Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Prof. Norman Sigallla King (aliyesimama) akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Kizengi (hawapo pichani) kilichopo kata ya
Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora baada ya kukagua ufikishaji na
upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini wakati wa ziara ya Kamati
hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga(aliyesimama mbele) akifafanua
jambo mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara ya Kamati
hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye
kijiji cha Mayamaya kilichopo Kata ya Zanka wilaya ya Bahi mkoani
Dodoma.
Meneja wa Kampuni ya Simu ya TTCL
Mkoa wa Tabora Bwana James Mlaguzi (wa kwanza kulia) akitoa taarifa kwa
wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa
huduma za mawasiliano viijini kwenye kijiji cha Kizengi kilichopo kata
ya Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Mhe. Mussa Ntimizi akisalimiana na wananchi wa kijiji cha
Kizengi kilichopo kata ya Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora wakati wa
ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa huduma za
mawasiliano vijijini.
…………………
Kamati ya Miundombinu ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano Tanzania inaendelea na ziara ya kukagua ujenzi wa
minara ya simu, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano
vijijini na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili kuhakikisha
kuwa wananchi wanapata na kutumia huduma za mawasiliano kwenye maeneo
mbali mbali nchini. Kamti hiyo imeendelea na ziara yake kwenye mikoa ya
Dodoma na Tabora ili kujiridhisha na utendaji kazi wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wa kufikisha mawasiliano kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu
wa UCSAF Eng. Peter Ulanga amesema kuwa Mfuko umetoa ruzuku kwa Kampuni
ya simu ya TIGO kujenga mnara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwa
wananchi.
Mfuko umetumia zaidi ya dola za marekani elfu arobaini na moja
na mia tano (41,500) ambapo ni sawa na zaidi ya shilingi milioni 85
kuipatia kampuni ya TIGO kujenga mnara ambao sasa unahudumia zaidi wa
wakazi 4,000 wa kijiji cha Mayamaya na vijiji vingine vya kata ya Zanka
wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambapo walikuwa hawana huduma za
mawasiliano na sasa wananufaika na uwepo wa huu mnara na wanapata huduma
za mawasiliano. Mnara huu ulikamilika mwezi Machi mwaka jana na kuanza
kutoa huduma ya mawasiiano kwa wananchi.
Naye mwakilishi wa kampuni ya simu
ya TIGO mkoa wa Dodoma mhandisi Hassan Said Gimbo wa kampuni hiyo
amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu waliofanya ziara ya
kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za
mawasiliano kuwa kampuni yao imekamilisha ujenzi wa mnara na sasa unatoa
mawasiliano kwa wananchi.
Pia ameongeza kuwa kampuni ya TIGO
inafuatilia mara kwa mara kwenye eneo hilo na kuhakikisha kuwa
mawasiliano yanapatikana. “Tunajitahidi kwa kiasi kikubwa kukarabati na
kuhakikisha kuwa pale mawasiliano yanapopotea au kuwa hafifu tunafanya
haraka kuyarudisha”, amesema mhandisi Gimbo.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Mhe. Mussa Ntimizi
ameipongeza Serikali kwa kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi
kupitia UCSAF ili kufikisha huduma za mawasiliano vijijini.
Mhe. Ntimizi
ameongeza kuwa kwa sisi wawakilishi wa wananchi tunaotoka vijijini
tunaelewa mahitaji na kiu ya wananchi ya kupata mawasiliano kwenye
makazi yao na umuhimu wa huduma nyingine za mawasiliano. “Ukiangalia
eneo kama hili halivutii kibiashara hivyo sio rahisi kwa kampuni za simu
kama hii ya TIGO kuja kuweka mnara wa simu hapa” amesema Mhe. Ntimizi.
Tumepata taarifa kuwa zaidi ya
vijiji vitano vyenye wakazi zaidi ya watu 4,000 wanapata mawasiliano
kupitia mnara huu wa TIGO.
“Kwa wananchi zaidi ya 4,000 kukosa
mawasiliano sio kitu kidogo na Mfuko huu unafanya kazi kubwa ya
kufikisha mawasiliano vijijini na Serikali inatumia gharama kubwa
kujenga minara ya simu za mkononi na kutoa huduma za mawasiliano
vijjijini, hivyo wahakikishe kuwa huduma za mawasiliano zinapatikana
muda wote”, amesema Mhe. Ntimizi.
Pia, ametoa rai kwa kampuni za
simu nchini kuboresha na kukarabati miundombinu ya mawasiliano na minara
yao ili wananchi waendelee kupata mawasiliano muda wote kwa kuwa
serikali inatoa fedha nyingi kwa maana ya ruzuku na kuwapatia kampuni za
simu ili ziweze kufikisha huduma za mawasiliano kwa wanachi muda wote.
Amesema kuwa huduma hizi zina
gharama kubwa sana na wananchi hawajui gharama kubwa ambayo Serikali
imeingia kutengeneza mnara huu ambazo ni kodi zao na hawaoni thamani ya
Serikali kuwaletea huduma hii. Wananchi muendelee kulinda miundombinu ya
mawasiliano na kusiwepo na wizi wa mafuta ya dizeli, mitambo na vitu
vingine kwa kuwa Serikali inatumia gharama kubwa kufikisha huduma za
mawasiliano vijijini ambapo ujenzi wa mnara mmoja unagharimu zaidi ya
shilingi milioni 200, hivyo kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake ili
kulinda miundombinu hii ya mawasiliano.
Tunaipongeza Serikali kwa kujenga
mnara kwenye kijiji chetu kwa kuwa tunapata mawasiliano na pale
yanapokuwa hayapatikani yanakatika wataalamu wa kampuni ya TIGO wanafika
na kurekebisha hali hii, “hakuna mawasiliano ya kampuni nyingine yoyote
zaidi ya hii ya TIGO kwenye eneo hili”, amesema mkazi wa kijiji cha
Mayamaya, Bwana Emmanuel Konyanza kilichopo kata ya Zanka wilaya ya
Bahi mkoani Dodoma.
Katika ziara hiyo ya Kamati kwenye
kijiji cha Kizengi kata ya Kizengi iliyopo wilaya ya Uyui mkoani
Tabora, Meneja wa TTCL mkoa wa Tabora Bwana James Mlaguzi ameihaidi
Kamati hiyo kuwa wataongeza upana wa masafa ya TTCL ili yaweze kufika
kwenye vijiji vya mbali zaidi kwenye kata ya Kizengi ndani ya kipindi
cha miezi miwili kuanzia sasa. Naye Diwani wa Kata hiyo Bwana Magindika
Lugaira Masaga akizungumza kwa niaba ya wananchi mbele ya wajumbe wa
Kamati hiyo amesema kuwa hapo mwanzo wananchi walikuwa na shida kubwa ya
mawasiliano.
Bwana Masaga anawashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kufanya
ziara na wanategemea kuwa huduma za mawasiliano zitaongezeka na kuwa
bora zaidi kwa kuwa mawasiliano ya minara ya kampuni nyingine sio mazuri
sana bali wanategemea mnara wa Halotel pekee ambao una masafa marefu na
kufikia wananchi walio wengi zaidi. hivyo mnara wa TTCL ukikamilika
utasaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi wa kata hii yenye vijiji saba
na wakazi 23,534.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment