Tuesday, September 26, 2017

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI ASIFU MPANGO MKAKATI WA UPATIKANAJI MAJI WILAYA YA IKUNGI

Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe akisalimiana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturumara baada ya kuwasili Mkoani Singida kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua Miradi ya vyanzo vya maji.
Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Ikungi mara baada ya kupita Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akielekea Manispaa ya Singida kwa ajili ya mapumziko, Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu
Baadhi ya Watumishi wa Wilaya ya Ikungi wakimsikiliza Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe mara baada ya kupita Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu (Kushoto) akimfatilia kwa makini Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Wilaya ya Ikungi, Mwingine ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ikungi Ndg Elieza
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Wilaya wakati wa ziara ya Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe
Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu.

Na Mathias Canal, Singida

Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida imepongezwa kwa kuanzisha mpango mkakati wa uundaji wa mamlaka ya maji katika makao makuu ya Wilaya ikiwa ni njia ya utatuzi ya changamoto inayowakabili wananchi wengi ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji Mhe Isack A. Kamwelwe wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Ikungi walioongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu na kuhudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu.

Kauli hiyo inajili wakati ambapo Naibu waziri Mhe Kamwelwe ameanza ziara ya kikazi Mkoani Singida ambapo atatembelea na kukagua Miradi ya Maji na vyanzo vya uboreshaji upatikanaji wa maji.

Alisema kuwa ili kunusuru kadhia inayowakumba wananchi katika Wilaya hiyo ya uduni wa upatikanaji wa maji ambapo wananchi wanaopata maji safi na salama ni 99,234 sawa na 32.2% ya wakazi wote 309,321 ni lazima kuwa na mbinu mbadala kupitia wataalamu wa maji na ushirikiano mkubwa na Serikali katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mhe Kamwelwe alisema kuwa Uongozi wa Wilaya ya Ikungi unatakiwa kupeleka mapema wizarani maombi ya uanzishaji wa Mamlaka ya maji mji wa Ikungi ili timu ya wataalamu kutoka Wizarani iweze kutumwa kwa ajili ya kujiridhisha.

Aidha, Alikiri kuwa wingi wa watu Katika eneo la Ikungi unakidhi kuanzisha mamlaka ya maji mji wa Ikungi kwani miongoni mwa sifa muhimu huwa ni pamoja na wingi wa watu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alisema kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ikungi si wa kuridhisha sababu ambayo inapalekea wananchi kwenda umbali mrefu na kutumia muda mwingi kupata huduma ya maji.

Alisema kuwa pamoja na kuwa na matanki ya maji ya mvua ambayo mengi yamejengwa katika taasisi za umma kama shule na vituo vya kutolea huduma za afya lakini bado changamoto ni kubwa kutokana na kuwepo kwa kipindi kirefu cha kiangazi (Miezi sita mpaka saba) na hivyo kufanya vyanzo vingi vya maji kutumika wakati wa msimu pekee.

Mhe Mtaturu alisema kuwa wakati wa kiangazi mifugo hupata maji kwenye malambo yaliyojengwa kwenye vijiji vyenye miradi ya maji ya bomba, Mabwawa na Malambo au visima walivyochimba wafugaji wenyewe.

Alisema pamoja na kuwepo kwa Mabwawa na malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo na shughuli zingine za binadamu katika sekta ya ujenzi na mahitaji ya majumbani lakini bado Wananchi wanahitaji malambo zaidi ili kupunguza makali ya upatikanaji wa maji.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu Alishukuru kwa ajili ya kupata fedha za kutengeneza miradi ya maji katika kata ya Sepuka, Kijiji cha Nkhoiree Kata ya Iseke na Kijiji cha Tewa Kata ya Ntuntu.

Pamoja na Shukrani hizo lakini pia Mhe Kingu alimuomba Naibu waziri huyo wa Maji na Umwagiliaji kusaidia utatuzi wa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa kijiji cha Igilansoni Kata ya Igilansoni kwani ni Kijiji kikubwa lakini kipo mbali na Vijiji vingine.

Hata hivyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 idara ya maji imepanga kuendelea kutoa huduma ya maji safi na salama na upatikanaji wa maji ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani na kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi kwa kuongeza idadi wananchi wanaopata maji safi na salama karibu na maeneo wanayoishi kwa kiwango cha 49% (June 2018).

MWISHO.

No comments:

Post a Comment