Thursday, September 7, 2017

ILEMELA YAENDELEA KUWA KIMBILIO LA MAFUNZO KWA HALMASHAURI NYINGINE NCHINI

Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imeendelea kuwa kimbilio la halmashauri mbalimbali nchini kwaajili ya kujifunza mbinu na mikakati inayoitumia kufikia mafanikio makubwa iliyonayo ndani ya muda mfupi.

Hayo yamekuja kufuatia ziara ya halmashauri ya wilaya Chato waliyoifanya leo kwa kufanya kikao na wataalamu wa manispaa hiyo kuwafundisha mbinu na mikakati katika kutekeleza shughuli za maendeleo na baadae kutembelea soko la kimataifa la biashara ya samaki Kirumba kabla ya kikao cha majumuisho ambapo makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato Mheshimiwa Thobias Kigwanamba mbali na kuishukuru Ilemela kwa kukubali kuwafundisha mbinu za ukusanyaji mapato, shughuli za kiwekezaji, uendeshaji wa soko la kimataifa la samaki, utoaji wa fedha kwa vikundi vya wanawake na vijana  ametaka kuimarishwa kwa mahusiano baina ya pande hizo mbili

‘…Tunawashukuru Ilemela kwa kukubali kutupokea na kushiriki nasi  katika shughuli zilizotuleta kwa manufaa ya wananchi wetu na halmashauri yetu ya Chato kikubwa tumekuja kujifunza na mapokezi yenu yanaashiria mtatuelekeza vizuri  kwa kile ambacho tumekifata kwenu na tunaomba sana ushirikiano huu uendelee usiishie kwa sisi kuja Ilemela …’ Alisema

Kwa upande wake Mstahiki meya wa halmashauri ya manispaa Ilemela Mheshimiwa Renatus Mulunga mbali na kuwakaribisha amesema kuwa mafanikio ya Ilemela yametokana na ushirikiano wa dhati baina ya viongozi wa wilaya hiyo kwa maana ya Mheshimiwa Mbunge Daktari Angeline Mabula, Mkuu wa wilaya, Mkurugenzi, madiwani na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa kufanya kazi pamoja katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo bila kujali tofauti zao

Akihitimisha mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga mbali na kuihakikishia halmashauri ya Chato ushirikiano amezitaka halmashauri nyengine kuja Ilemela kujifunza wakati wowote kwa kile watakachoona kinafaa kwa kuamini kuwa maendeleo ya wananchi yataletwa kwa viongozi kuwajibika na kushirikiana kama ambavyo kauli ya manispaa ya Ilemela inavyosema

‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
07.09.2017

No comments:

Post a Comment