Saturday, September 30, 2017

Halmashauri 7 zaingia matatani fedha za barabara

MWENYEKITI WA BODI YA MFUKO WA BARABARA (RFB), JOSEPH HAULE

HALMASHAURI saba ziko matatani baada ya kubainika kutumia Sh. milioni 359 zilizotengwa kwa ajili ya barabara kununulia madawati na kujenga maabara huku zingine tatu zikingia mikataba yenye kutia shaka. 

Halmashauri hizo ni Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera, Ushetu (Shinyanga), Masasi na Nanyumbu (Mtwara), Kilolo (Iringa) na Songea mkoani Ruvuma. 

Wakati halmashauri hizi zikitumia fedha kinyume cha maelekezo, zingine tatu za Monduli, Tanga na Mtwara zilibainika kuwa na mikataba feki iliyosababisha matumizi ya Sh. milioni 87. 05 kwa matumizi yao. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Joseph Haule, aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kuwa kutokana na hali hiyo, ametoa siku 30 kwa halmashauri hizo hadi Oktoba 30, mwaka huu, kuhakikisha zinarejesha fedha hizo ili zitumike katika ujenzi wa barabara kama zilivyopanga. 

Alisema halmashauri zingine zimejaza kazi hewa kwa kutoa mchanganuo wa fedha za barabara na kudai kwamba zimetumika katika kazi hizo hewa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 

"Ninawashangaa sana hawa watu hii serikali ya awamu ya tano si ya kudanganya hata kidogo," alisema Haule.
Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha wanatekeleza agizo la kurejesha fedha hizo ndani ya muda waliopewa kufanya hivyo, kabla ya hatua stahiki hazijachukuliwa kulingana na kile walichokifanya.
 

Pia alisema halmashauri ambazo zimevurunda ujenzi wa barabara na madaraja ambayo yamezolewa na maji kutokana na kuwa chini ya kiwango, wasiajiriwe katika sekta ya ujenzi. 

"Tumeanzisha Tarura (Wakala wa Barabara Vijijini) kwa makusudi ambayo haitaji wahandisi vihiyo. Wale waliobainika halmashauri zao zina kashfa basi hawatakiwi," alisema Haule. 

Alisisitiza kuwa wahandisi ambao hawajasajiliwa wasiajiriwe kwa ajili ya kufanya kazi kwa sababu wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mikakati ambayo imewekwa kwa ajili ya kuhakikisha barabara zinaboreshwa. 

NYARAKA ZAPOTEA
 
Haule alisema nyaraka za malipo ya Sh. milioni 24.5 katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro zinadaiwa kupotea na kwamba kasi yao isiyoridhisha ya utekelezaji wa miradi ya matengenezo ya barabara na matumizi ya fedha za mfuko wa barabara ni kinyume cha mkataba wa utekelezaji wa kazi.
 

Aliitaka Halmashauri hiyo na ile ya wilaya ya Kondoa kuhakikisha ifikapo Oktoba 30, madaraja yaliyojengwa chini ya kiwango yanajengwa kwa fedha zao wenyewe kwa kuwa serikali tayari ilishatoa fedha awali.

Naye, Meneja wa Bodi ya Barabara, Eliud Nyauhenga, alisema bodi imeajiri wahandisi kufuatilia fedha za mfuko wa barabara ndiyo maana upungufu huo umebainika.
 

Hata hivyo, alisema ana imani madudu hayo hayataonekana kwa sababu Tarura imeanza kazi na haitakubali wahandisi ambao ni wabadhirifu wa fedha za umma. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema Gairo ni moja ya wilaya zilizofanya vibaya kwenye fedha za mfuko wa barabara.

Alisema atahakikisha wote walioshiriki katika ubadhirifu huo wanachukuliwa hatua hata kama wamehamishwa na kutaka barabara zote zinazojengwa kuwa kwenye viwango vinavyotakiwa.

No comments:

Post a Comment