Mwenyekiti wa
Kamati Maalum ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mhe. Dotto Mashaka Biteko
Asilimia 80 ya Madini ya Tanzanite
yanayochimbwa nchini hutoroshwa nje ya nchi kwa njia ya magendo na
asilimia 20 tu ndiyo inayoingizwa katika mfumo wa kodi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa
Kamati Maalum ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite Mhe. Dotto Mashaka Biteko wakati wa uwasilishwaji wa taarifa hiyo leo, katika viwanja vya Bunge
Mjini Dodoma.
“Biashara ya Tanzanite imegubikwa
na wizi mkubwa ambapo takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1998 ni kilo
13.2 tu za Tanzanite zimezalishwa nchini, sawa na kuzalisha gramu 700 za
Tanzanite kwa mwaka kwa kipindi chote cha miaka 19,” amefafanua Mhe.
Biteko.
Biteko amesema kuwa Kamati yake
imebaini vichochoro 400 vinavyotumika kutorosha Tanzanite nchi jirani na
kuikosesha Tanzania mapato yanayotokana na madini hayo yanayotoroshwa
kinyemela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Kamati Maalum ya Kuchunguza Biashara ya Almasi Mhe. Musssa Azzan Zungu
amesema kuwa madini ya Almasi yamekuwa yakisafirishwa nje ya nchi kama
malighafi ambapo huko husafishwa na kukatwa vizuri na baadae kuuzwa kwa
gharama kubwa.
Usafirishwaji wa madini hayo kama
malighafi Tanzania imepoteza fedha nyingi ambapo kwa nchi ya Botswana
inauza Almasi yake ndani ya nchi kwa Dola 1900 na Tanzania tunauza nje
ya nchi kwa Dola 300.
Vile vile Mhe. Zungu amesema
kumekuwepo a udangabyifu mkubwa katika usafirishaji wa madini ya Almasi
nje ya nchi ambapo Kamati yake imegundua kuwa kuna Almasi ilithaminishwa
hapa nchini ambayo ilikuwa na thamani ya Dola Milioni 15 lakini iliuzwa
Dola Milioni 10 nje ya nchi.
Aidha, Kamati zote hizo
zimeishauri Serikali kupitia upya mikataba ya madini ambayo Serikali
imeingia na makampuni ya madini yanayoisababishia Serikali hasara kubwa.
Vile vile wameshauri Serikali
kuleta wawekezaji watakaoleta mitambo ya kuchuja madini ambayo itaongeza
thamani ya madini na kuuzwa kwa gharama ya juu.
Nae, Spika wa Bunge la Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amesema kuwa Watanzania waungane
katika kutetea maslahi ya nchi hasa katika masuala ya madini.
akitolea mfano Mhe. Ndugai alisema
“Zipo koo ambazo zinatofautiana lakini kuna kipindi ambacho huungana
katika kutetea maslahi ya koo zao”.
Aidha, Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa amesema kuwa zaidi ya makampuni 10 yamejitokeza kujenga mitambo
ya kuchujia madini nchini, Hivyo madini yote yatakuwa yakichenjuliwa
hapa nchini mara mitambo hiyo itakapoanza kufanya kazi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema
kuwa ushauri wote uliotolewa na kamati zote mbili utafanyiwa kazi kwa
muda muafaka tena kwa kipindi kifupi.
Kamati maalum za kuchunguza
biashara ya Tanzanite na Almasi ziliundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania mapema Juni mwaka huu, baada ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kupokea taarifa ya kamati ya pili ya kuchunguza mchanga
wa madini ya dhahabu (makinikia) na kulitaka Bunge la Jamhuri ya
Muungano nao kufanya kitu juu ya madini yanayosafirishwa nje ya
nchi.
No comments:
Post a Comment