WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali italipa madeni yote ya watumishi ambayo yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali.
“Mheshimiwa
Rais, Dk. John Pombe Magufuli alisitisha malipo sababu ya zoezi la
kubaini watumishi hewa, sasa kazi hiyo imeshakamilika, yale
yaliyobainika kuwa ni halali yatalipwa. Tunataka watumishi mfanye kazi
ya kuwahudumia wananchi kwa bidii,” alisema.
Ametoa
kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika
kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.
Akiwa
katika wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui, Waziri Mkuu alielezwa
na baadhi ya wabunge wa mkoa huo kwamba kuna watumishi ambao
walihamishwa kutoka manispaa kwenda wilaya za jirani lakini hawajalipwa
fedha zao kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Kwa
nyakati tofauti, Waziri Mkuu ambaye ameweka utaratibu wa kukutana na
watumishi wa umma kila anapofanya ziara za kikazi mikoani, aliwaeleza
watumishi wa wilaya hizo kwamba Serikali imeanzisha mfumo wa
kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao
unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.
“Hivi
sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni
ya matibabu, ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa
kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi
kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete
madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu,” alisema.
Akifafanua
utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao
kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa
Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa na kwamba unasaidia kutunza,
kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu
mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama
kustaafu.
Akifafanua
kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali
imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri
kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
“Hii
imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili
imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa
za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti
kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine
alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo,” alisema.
“Mimi
nimekuwa kwenye utumishi wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu
anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa
maafisa utumishi kuona kama kuna watumishi wanastahili kupandishwa
madaraja, watume taarifa zao mapema (kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi
ili waingizwe kwenye mfumo huu, kisha wawaandikie barua za kuwajulisha
wahusika. Hata barua ikichelewa kumfikia mtumishi, mshahara wake
hautachelewa na kwa njia hii tutaepuka kuweka madeni yasiyo na tija,” alisema.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao wajibu wao wa
kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na akasisitiza kuwa Serikali
haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.
“Napenda
kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi
lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye
mwadilifu na mla rushwa. Tukikukamata hatuundi tume kwa sababu tume nazo
zinamaliza fedha tu. Tukiwa na ushahidi wa kutosha, tunamalizana
hapohapo,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment