Tuesday, August 8, 2017

Waziri Hamad Rashid Aiasa Benki ya Kilimo

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed akihimiza jambo kwa uongozi wa Benki ya Kilimo.
Na Mwandishi wetu, Lindi
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed ameiasa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuwezesha wakulima ili waweze kuchangamkia fursa za kuuza mazao ya kilimo nje ya nchi ili kuwaongezea kipato wakulima hao.
Waziri Hamad aliyasema hayo alipolitembelea Banda la TADB katika Viwanja vya Ngongo mjini Lindi wakati wa Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea mjini humo.
Mhe. Hamad alisema kuwa Tanzania inapata fursa nyingi za masoko nje ya nchi kwa mazao mbalimbali ikiwemo zao la karafuu, korosho na mazao ya mikunde ikiwemo dengu na mbaazi zinazotakiwa sana nchini India na Arabuni.
“Naiomba Benki ya Kilimo kuwawezesha wakulima wanaolima kibiashara ili kuchangamkia fursa za masoko kwa mazao ya kimkakati yakiwemo zao la karafuu, korosho na mazao ya mikunde ikiwemo dengu na mbaazi ambazo nchi nyingi marafiki wanahitaji,” alisema Mhe. Hamad.
Aliongeza kuwa wizara yake inaletewa maombi mengi ya mazao kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nchi hizo.
Kwa mujibu wa Waziri Hamad kuna wafanyabiashara wa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu wanaohitaji zaidi ya kontena mbili za korosho kwa wiki hivyo Benki ya Kilimo ina wajibu wa kuwezesha wakulima ili waweze kuchangamkia fursa hizo.
“Naamini Benki ikiwawezesha wakulima wanaweza kuchangamkia fursa za masoko ya nje ikiwemo ya wafanyabiashara kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu wanaohitaji zaidi ya kontena mbili za korosho kwa wiki,” aliongeza.
Akizungumza wakati wa akipokea ugeni huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa TADB ni kuchagiza juhudi za serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa katika kutekeleza hayo Benki ya kilimo imedhamiria na kujizatiti katika kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.
“Lengo letu ni kuhakikisha tuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema Bw. Assenga.
Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa sekta hizo ili kuongeza tija sekta hizo ili kupambana na umaskini nchini.

No comments:

Post a Comment