Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji jumanne Mtaturu
Wanasiasa
hasa wasomi na wale wenye ushawishi mkubwa wametakiwa kuacha kulalamika
na kutoa kauli ambazo hazitawasaidia wananchi katika kuwatatulia
matatizo na kero zao mbalimbali waungane na serikali katika juhudi
zinazoonekana za kuleta maendeleo.
Rai
hiyo imetolea na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu jana
wakati wa uzinduzi wa Ligi ya mpira wa miguu ambayo ina lengo la
kuutambulisha kwa wananchi na wadau mbalimbali mfuko wa elimu wa wilaya
hiyo ili wahamasike kuuchangia.
Mtaturu
amesema baadhi ya wanasiasa maarufu wamekuwa wakitumia muda mwingi
kueleza matatizo na kero za wananchi bila ya kuonyesha suluhisho au
kusaidia kutatua kero hizo jambo ambalo halimsaidii mwananchi kwa namna
yoyote.
“Baadhi
ya Wanasiasa utawaona mstari wa mbele kutajataja kero za wananchi
wanapokuwa majukwaani wakati hawatoi mchango wowote wa kutatua kero hizo
au hata kueleza mapendekezo ya nini kifanyike, acheni kufanya hivyo
kwakuwa mna watonesha vidonda wananchi, kusema sema hakusaidii, onyesha
njia ya kumsaidia mwananchi kama ambavyo sisi tunafanya leo katika sekta
ya elimu”, amesema Mtaturu.
Amesema
Sekta ya elimu Wilayani humo inakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu,
vyumba vya madarasa na maabara ambapo mfuko wa elimu una mpango wa miaka
mitatu yaani 2017-2020 wa kukusanya zaidi ya bilioni tatu
zinazohitajika kutatua changamoto hizo.
Mtaturu
amesema kati ya mahitaji ya maabara 90 wilayani humo, zipo maabara nne
tu na kwa kuanzia mfuko huo umeweka malengo ya kuhamasisha wananchi
kufyatua tofali elfu kumi kwa kila kata ili ziweze kutatua changamoto
hiyo.
Ameongeza
kwa kuwapongeza wananchi, viongozi na madiwani waliojitokeza kuchangia
mfuko huo ambapo yeye amechangia mifuko mia moja ya simenti, wadau na
wananchi walitoa mifuko 194 ya simenti, fedha taslimu laki nane, ahadi
milioni moja laki tisa, mchanga ‘trip’ tano na moramu.
“Nawashukuru
sana madiwani wa Ikungi na wananchi kwakweli tumeanza vizuri na nina
imani mfuko huu wa elimu utasaidia kupunguza changamoto za sekta ya
elimu wilayani humu, tunaendelea kukaribisha wadau mbalimbali, lakini
pia wananchi msisite kama una mchanga leta, una siment hata maji tu ni
mchango pia tusikariri mchango lazima ni fedha”, ameongeza.
Mgeni
rasmi wa ufunguzi wa Ligi hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt
Angelina Mageni Lutambi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt
Rehema Nchimbi amewapongeza wananchi wa Ikungi kwa kuupokea mfuko huo
kwa hamasa kubwa.
Dkt
Lutambi amesema mfuko huo utaboresha elimu hasa ujenzi wa maabara
ambazo ni msingi wa maendeleo ya sayansi ambapo bila kufanya vizuri
katika sayansi wilaya hiyo haitaweza kujikomboa katika viwanda na
kuelekea uchumi wa kati.
“Ukombozi
wa nchi yoyote bila sayansi haiwezekani, Ikungi mkiboresha mazingira ya
hawa wana sayansi wanafunzi mnatengeneza jamii ya wanasayansi ambao
wataikomboa wilaya yetu kwa kuweka ubunifu kwenye viwanda ambavyo hukuza
uchumi kwa haraka”, amesisitiza.
Ameongeza
kuwa Ligi hiyo isaidie kuwaunganisha wananchi hao na kuchangamkia
katika kuchangia maendeleo ya elimu wilayani humo, aidha ameitaka
halmashauri kusimamia mfuko huo kwa umakini ili uweze kutekeleza
majukumu yaliyotarajiwa.
Naye
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Daudi Magiligimba amesema
michezo huleta amani na kusaidia katika kuhamasisha maendeleo hivyo basi
ligi hiyo isaidie kuhamasisha kwa amani uchangiaji wa mfuko huo.
Wakati
huo huo ACP Magiligimba amewapongeza wananchi wa Ikungi na Mkoa wa
Singida kwa kushirikiana na jeshi la polisi katika kupunguza wahalifu na
uhalifu.
Amesema
uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaoupata
kutoka kwa wananchi licha ya uhalifu wa ubakaji ukionekana kuongezeka
hivyo amewataka wananchi kuendela kutoa ushirikiano ili ubakaji uishe.
ACP
Magiligimba amewataka wananfunzi kuacha vitendo vya ngono na vijana
kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kwakuwa yote hayo huharibu maisha
yao bali wakazane katika masomo na michezo.
Ligi
ya mpira wa miguu Wilayani Ikungi yenye lengo la kuhamasisha wananchi
na wadau kuchangia mfuko wa elimu imeanza rasmi jana na inatarajiwa
kuhitimishwa mwezi Septemba ambapo zaidi ya timu 69 zitashiriki.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi akifyatua
tofali wakati wa uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha
mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu kumi yanatarajiwa
kufyatuliwa kwa kila kata.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akifyatua tofali wakati wa
uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu
wilayani humo, Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila
kata.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba akizungumza
wakati wa uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa
elimu wilayani humo, Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa
kila kata.
Sehemu ya mchango ya simenti kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji
Mtaturu pamoja na wadau mbalimbali ambapo Matofali elfu kumi
yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata ili kutunisha mfuko wa elimu
Wilayani humo wenye lengo la kutatua baadhi ya changamoto ya ukosefu wa
maabara na vyumba vya madarasa.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi akimkabidhi
bahasha yenye shilingi laki mmoja kati ya wanafunzi 16 wa Sekondari ya
Ikungi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika matokeo ya kidato cha
sita kama sehemu ya kuhamasisha wanafunzi na walimu kufanya vizuri,
aidha wanafunzi hao walipatiwa shilingi laki moja kila mmoja huku walimu
wakipatiwa motisha ya shilingi milioni moja.
Baadhi ya wananchi wakijitolea kufyatua tofali ambapo Matofali elfu
kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata ili kutunisha mfuko wa elimu
Wilayani humo wenye lengo la kutatua baadhi ya changamoto ya ukosefu wa
maabara na vyumba vya madarasa.
No comments:
Post a Comment