Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imekutana
Jumapili Julai 30, 2017 katika Ukumbi wa Hosteli za TFF, zilizopo Uwanja
wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam yaliko Makao Makuu
ya shirikisho.
Kikao
hicho, kimepitisha mambo mbalimbali ambako miongoni mwake ni mabadiliko
ya Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Miongoni mwa kanuni
ziliguswa ni ya kuhusiana na kujali afya za wachezaji pamoja na mikataba
wanayoingia na klabu.
Hivyo,
TFF imeagiza msimu wa 2017/18 mchezaji atayesajiliwa hatapewa leseni ya
kumruhusu kucheza mashindano husika kama vile Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania (VPL), Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kama
hatakamilisha masharti makuu matatu kwa mujibu wa kanuni.
Masharti
hayo ni kukatiwa Bima ya Matibabu, Kuidhinishwa afya yake ambayo mara
baada ya fomu yake kupitishwa na Kamati ya Tiba ya TFF kwa mujibu wa
Kanuni ya 18 (1) ya Ligi Kuu na Mkataba wake wa maandishi ‘hardcopy’
kuwasilisha TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 69 (8) ya Ligi Kuu.
Kama
kuna timu haitakidhi japo sharti moja kati ya hayo, basi mchezaji wake
hatapewa leseni ya kucheza kwa msimu husika. Kaimu Rais wa TFF, Wallace
Karia, akifunga hoja hiyo, alisisitiza akisema: “Wakati huu hatutaki
siasa. Tusimamie kanuni hizi, hatutaki kuleta mchezo msimu huu.”
Hayo
yamekuja baada ya klabu kutakiwa kuwawekea Bima ya Matibabu kwa mujibu
wa kanuni ya 18 (1) inayosema: “Kila Klabu ina wajibu wa kuwawekea
wachezaji wake bima ya matibabu na fidia kutokana na ajali michezoni.
Klabu itakayokiuka kanuni hii itakuwa imepoteza sifa ya kuwa klabu ya
Ligi Kuu, na usajili wa wachezaji wa timu yake hautathibitishwa na
haitashirikishwa katika Ligi Kuu.
Kuhusu
Mikataba kwa mujibu wa Kanuni ya 69 (8), Kamati ya Utendaji
imekubaliana kwamba: “Mikataba yote ya wachezaji ambao haujasajiliwa na
kuthibitishwa na TFF, hautatambuliwa.”
Kadhalika,
kuhusu wachezaji wa Kigeni kwa mujibu wa Kanuni ya 57 (5), kitasomeka
kama ifuatavyo: “Mchezaji ye yote wa kigeni anayesajiliwa katika Ligi
Kuu atalipiwa ada maalumu ya Sh milioni mbili (Sh 2,000,000) kwa msimu
kwa mchezaji mmoja ili usajili wake uweze kuthibitishwa na kuruhusiwa
kucheza.
Gharama za awali zilikuwa ni dola 2,000 za Marekani (sawa na Sh. 4.5 milioni.) kwa mchezaji mmoja.
Kadhalika,
sasa kwa mujibu wa kanuni ya 13 (6) Klabu Mwenyeji itakuwa na nafasi ya
kuweka mpaka mabango 10 ya Mdhamini/Wadhamini wake. Ukubwa wa bango
moja lile lenye vipimo vya 6m x 1m.
Kama
timu ni mgeni katika mchezo husika, ana uwezo kufanya makubaliano na
mwenyeji wake akampa nafasi katika hayo 10 ambayo yameruhusiwa kikanuni.
Aidha,
Kanuni ya 14 imeongezwa kipengele kimoja. Kanuni ya 14 (48) Klabu ina
wajibu wa kushirikiana na mdhamini wa matangazo ya televisheni ikiwemo
kupata picha za wachezaji na benchi la ufundi kwa ajili ya maandalizi ya
mechi zao.
Na
Kanuni 14 (49), inasema: TFF/TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wo wote
wa taratibu za mchezo kama zilivyoanishwa kwenye Kanuni ya 14 kwa kutoa
onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia Sh. 200,000 (lakini mbili)
mpaka Sh. 300,000 (laki tatu), na/au kufungia mchezo isiyozidi mitatu
(3) au kipindi kisichozidi miezi mitatu (3) kwa mchezaji, kiongozi au
timu.
Katika
hatua nyingine, Kamati ya Utendaji imeridhishwa na maandalizi ya
Mkutano Mkuu ujao wa TFF ambako pamoja na mambo mengine utakuwa na
ajenda ya Uchaguzi Mkuu wa shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 12,
mwaka huu.
Mjumbe
wa FIFA, Solomon Mudege alikuwa nchini kwa siku ya Jumamosi ambako
alipata fursa ya kuzungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe; Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo,
Yussuph Singo pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF wakiongozwa
na Kaimu Rais Wallace Karia.
Mara
baada ya kupata maelezo ya kuridhisha kutoka kwa wanafamilia hao wa
mpira wa miguu ambao baadhi yao alikutaa nao mmoja baada ya mwingine,
alibariki mchakato wa uchaguzi uendelee na Kamati ya Utendaji imetangaza
kuwa utafanyika Ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma.
Mudege
alikuwa nchini kuangalia hali maendeleo ya mpira wa miguu nchini hasa
katika utawala, lakini kwa kuwa uongozi uliokaimu madaraka umefuata
taratibu, kanuni na sheria tangu mwanzo, mjumbe huyo aliridhia mchakato
wa uchaguzi na shughuli nyingine ziendelee kama zilivyopangwa.
MATOKEO YA MWISHO USAILI TAFCA, KAMPENI ZAANZA
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania
(TAFCA), Ramadhani Mambosasa ametangaza orodha ya majina sita ya mwisho
ya wagombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika
Agosti 12, mwaka huu.
Kwa
mujibu Mambosasa, wagombea hao kwa sasa hawana budi kuendelea na
kampeni hadi Agosti 9, mwaka huu ambako uchaguzi huo umepangwa kufanyika
kufanyika Agosti 10, mwaka huu mjini Dodoma.
Waliopitishwa
katika orodha ya mwisho kuwania nafasi mbalimbali za uongozi – ngazi ya
taifa ni pamoja na Kidao Wilfred, Lister Manyara, Michael Bundala,
Dismas Haonga, Jamhuri Kihwelo, George Komba, Samuel Moja na Maka
Mwalwasi na Mohammed Tajdin.
Nafasi
zinazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu
Msaidizi, Mweka Hazina, Wajumbe wa Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati
ya Utendaji.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment