Tuesday, August 1, 2017

Tanzania na Uganda kushirikiana kupeleka umeme vijiji vya mpakani

Na Veronica Simba, Kagera
 Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) wa kupeleka umeme kwenye Vijiji vya Mpakani mwa nchi hizo.

Hati ya Makubaliano hayo ilisainiwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga akiwakilisha Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania) na Waziri wa Nishati wa Uganda, Dk. Simon D’Ujanga, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa nchi hizo kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika mjini Bukoba, wilayani Kagera.

Makubaliano ya msingi katika Hati iliyosainiwa ni utekelezaji wa Mradi wa kupeleka umeme kwenye vijiji vya Nangoma, katika eneo lililopo mpakani mwa Tanzania na Uganda na vijiji vingine vya maeneo hayo kwa kutokea upande wa Tanzania.

Akifafanua zaidi kuhusu makubaliano husika, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, ambaye pia alishiriki Mkutano huo mkubwa, alisema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini kwa upande wa Tanzania (REA-Tanzania) utahusika katika kugharamia ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kufikisha umeme katika eneo la mpakani, umbali wa kilomita 0.8 kwa gharama ya Dola za Marekani 36,923.05.

Aidha, aliongeza kuwa, kwa upande wa Uganda, Wakala wa Nishati Vijijini wa nchi hiyo (REA-Uganda) utahusika kugharamia ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 umbali wa kilomita 7.5 kutoka eneo la mpakani hadi katika vijiji vya Bukwali Gamuli, Bushungulu, Nangoma, Omurushenye, Mizinda na Lukunyu kwa gharama ya Dola za Marekani 724,239.06.

Alieleza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), litakuwa na jukumu la kuuza umeme kulingana na Mkataba wa kusambaza umeme utakaosainiwa kati yake na Shirika la Umeme la Uganda.

Vilevile, alisema kuwa, REA-Tanzania itashiriki katika kusaidia upatikanaji wa Mkandarasi atakayehusika na ujenzi wa Mradi kwa upande wa Uganda.

Katika Mkutano huo pia, masuala mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda, katika sekta ya nishati yalijadiliwa ambapo ilielezwa kuwa, mwaka 2014, Serikali hizo mbili zilisaini makubaliano (Bilateral Agreement) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kuzalisha umeme wa Murongo-Kikagati wa Megawati 14 kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Mradi mwingine wa ushirikiano katika sekta ya nishati, uliojadiliwa katika Mkutano huo ni wa kuzalisha umeme wa Nsongezi wa Megawati 35, ambapo ilielezwa kuwa, Serikali za Tanzania na Uganda zina nia ya kutekeleza Mradi huo kwa kutumia chanzo cha maji ya Mto Kagera ambao upo mpakani mwa nchi hizo.

Wataalam wamependekeza kuwa, hatua muhimu za utekelezaji wa miradi kama vile kufanya Upembuzi yakinifu wa Mradi, upatikanaji wa Mshauri Mwelekezi na Mwendelezaji wa Mradi, zifanyike kwa Ubia, chini ya uongozi wa Serikali ya Tanzania na Uganda.

Masuala mengine ya ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Uganda katika maeneo ya Mpakani, yaliyojadiliwa katika Mkutano huo wa Mawaziri ambao uliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Tanzania) ni kilimo na uvuvi, maji, ardhi pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.

Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka nchi hizo mbili wanaoshughulika na masuala ya ushirikiano katika maeneo ya Mpaka, uliofanyika Julai 28, mwaka huu mjini Bukoba.

No comments:

Post a Comment