Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Mhandisi Gerson Lwenge
KILIMO ndiyo
Msingi wa Uchumi wa Taifa letu ambapo takribani asilimia 70 ya
Watanzania hutegemea sekta hiyo kama shughuli kuu ya Kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba Nchi
yetu ina eneo kubwa linalofaa kwa Kilimo takriban Hekta Milioni 29.4,
ni Hekta 290,000 tu, sawa na Asilimia Moja (1%) zinazotumika kwa Kilimo
cha Umwagiliaji Maji.
Kwa maana hiyo, Kilimo cha Umwagiliaji
kinayo nafasi kubwa ya kuwezesha kufikia Mapinduzi ya Kijani kwa kuwa
kinatuhakikishia uzalishaji endelevu wa mazao badala ya kutegemea mvua
ambazo hazina uhakika wa kiasi na wakati wa kunyesha katika msimu.
Serikali imekusudia kuongeza eneo la
umwagiliaji kufikia hekta 1,000,000 katika skimu za wakulima wadogo, wa
kati na wakubwa ifikapo mwaka 2020, ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza
uzalishaji wa Mazao ya chakula na biashara na kuongeza tija katika
kilimo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Mhandisi Gerson Lwenge akizungumza na wananchi mara baada ya kytembelea banda la Wizara hiyo wakati wa Maonesho ya Nanenane katika viwanja vua Ngongo Manispaa ya Lindi anasema hadi mwezi Machi 2017, eneo
linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 461,326 kwa mwaka 2015/2016 na
kufikia hekta 468,338.
“Eneo hilo linachangia asilimia 24 ya
mahitaji yote ya chakula nchini kwa sasa, ambapo hekta milioni 2.3 zina
uwezekano mkubwa, hekta milioni 4.8 zina uwezekano wa kati na hekta
milioni 22.3 zina uwezekano mdogo” anasema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi Lwenge anasema katika mwaka
20176/18, Serikali inatarajia kutekeleza Mpango wa miaka 5 wa Programu
ndogo ya Umwagiliaji iliyolenga katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu
katika skimu na mabwawa ya umwagiliaji.
Waziri Lwenge anasema katika awamu hiyo,
Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika skimu 176,
ukarabati wa skimu 205, ukarabati wa mabwawa 30 na kujenga mabwawa mapya
40 ili kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na
matumizi mengine kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lwenge anasema
Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wakulima na wataalam kuhusu
usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji na kusajili vyama
vipya 100 vya wamwagiliaji katika skimu za wakulima wadogo; na
kuimarisha vyama 442 vya umwagiliaji vilivyopo.
Aidha Mhandisi Lwenge anasema Serikali
imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuendeleza skimu za
umwagiliaji za wakulima wadogo kwa awamu tatu katika Halmashauri 68
nchini.
Anasema kuwa hadi kufikia mwezi Machi
2017, ukarabati na ujenzi wa skimu 45 za awamu ya kwanza umekamilika na
utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi unahusisha ujenzi na ukarabati wa
skimu 63 ambapo ukarabati na ujenzi wa skimu 43 unaendelea; na taratibu
za kuwapata Wakandarasi wa skimu 20 zilizobaki zinaendelea katika
Halmashauri husika.
“Katika mwaka 2016/2017, Wizara kwa
kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 32 imeendelea kusimamia ukarabati
na uboreshaji wa skimu 45 za umwagiliaji za awamu ya kwanza zenye jumla
ya hekta 13,722 na hivyo kumeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta
461,326 hadi kufikia hekta 468,338” anasema Waziri Lwenge.
Serikali inaendelea kupitia Mpango
Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo
yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo kazi hiyo inatarajia
kukamilika katika mwaka 2018/2019.
Kukamilika kwa Mpango huo kutasaidia
kuleta Mapinduzi ya Kijani nchini ambayo yanahitaji matumizi ya
utaalamu, mbegu bora, mbolea, madawa, zana bora za kilimo pamoja na
kuongeza eneo la Kilimo cha Umwagiliaji.
Aidha Mpango huo umekusudia kuweka
mazingira mazuri ya kuongeza Uzalishaji katika Kilimo; kuongeza Pato la
Mkulima; kupunguza Umaskini Vijijini na kushirikisha Sekta Binafsi
kuleta uhakika wa Chakula katika Kaya.
No comments:
Post a Comment