Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amefungua Mashindano ya Mbio za Baiskeli na Ngoma za Asili Mjini Bariadi(Simiyu Jambo Festival) ambayo yamehudhuriwa na Maelfu ya Wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mashindano hayo ya mbio za baiskeli yamehusisha kilometa 200 wanaume, kilomita 80 wanawake ambapo pia walemavu waliweza kushindania katika umbali wa kilomita tano.
Akizungumza baada ya kufungua mashindano hayo Dkt.Tulia pamoja na kuupongeza Mkoa wa Simiyu kuandaa mashindano hayo amesema, ipo michezo nchini haijapewa kipaumbele lakini ikitumiwa vizuri inaweza kutoa ajira ukiwemo mchezo wa mbio za baiskeli; ambapo ametoa wito kwa viongozi wa mikoa mingine pia kuwekeza katika michezo mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kupata kipato.
“Lililofanyika Simiyu ni jambo jema sasa hivi watu watakuwa wanajua kuwa wakijifua vizuri kwenye baiskeli na ngoma za jadi wanakuja kushiriki mashindano ya Baiskeli na ngoma Simiyu, nitoe wito kwa viongozi wengine kufikiria mambo mengine yanayoweza kuwasaidia wananchi katika maeneo yao kupata ajira na kujipatia kipato” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema mkakati wa mkoa huo ni kurasimisha tamaduni zote na kuhusianisha na shughuli za Utalii ndani ya mkoa huo.
“Position(Nafasi) ya Mkoa wa Simiyu kwenye nchi ni kukuza tamaduni na sanaa zetu kama moja ya eneo litakalotuunganisha na sekta ya Utalii, tumezungukwa na mapori ya akiba na mbuga za wanyama, tungehitaji watalii wanapokuja kwenye maeneo hayo wapate ladha ya tofauti kiwemo utamaduni wa Mtanzania”
Mtaka ameongeza kuwa wasanii wote watatambuliwa na baadae kujengewa uwezo kupitia watalaam wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Kitivo cha sanaa),Chuo cha Sanaa Bagamoyo na vyuo vya michezo ili waweze kufanya kazi zao kibiashara na kuimarisha uchumi wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Food Products,Mhe.Salum Khamis ambaye ndio Mdhamini wa mashindano ya Baiskeli na ngoma za Asili (Simiyu Jambo Festival) amesema ataendelea kudhamini mashindano kama hayo Mkoani Simiyu ili kuwawezesha wananchi kuinua kipato kupitia vipaji vyao.
Naye mshindi wa kwanza mbio za kilometa 80 (wanawake) Raulensia Luzuba kutoka Mwanza ameomba mashirika na makampuni mbalimbali kuwadhamini ili waweze kujengewa uwezo na kuandaliwa kushiriki katika mashindano ya Kimataifa.
Masunga Duba mshindi wa mbio za kilometa 200(wanaume)kutoka Simiyu amesema pamoja na wafadhili kudhamini mashindano wawasaidie pia wachezaji kupata baiskeli za kisasa zitakazowasaidia kwenda kwa kasi inayotakiwa.
Mashindano ya baiskeli Mkoani Simiyu yameshirikisha wachezaji kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga,Arusha na Mbeya, ambapo ushindi kwa upande wa wanaume umechukuliwa na Hamisi Hussein(Arusha) ambaye amejishindia pikipiki, wa pili ni Masunga Duba(Simiyu) kitita cha shilingi 1,000,000/= wa tatu Richard Laizer(Arusha) .shilingi 500,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa 15.
Kwa upande wa wanawake mshindi wa kwanza Raulensia Luzuba kutoka Mwanza amejipatia shilingi 500,000/=, mshindi wa pili Tatu Malulu(Mwanza) shilingi 400,000/= na wa tatu ni Vumilia Mwinamila(Simiyu) shilingi 300,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa 10.
Walemavu mshindi wa kwanza Emmanuel Mtemi amejipatia shilingi 200,000/= wa pili Masunga Sendama shilingi 150,000/= na wa tatu Saguda Sospeter shilingi 100,000/=wote kutoka mkoa wa Simiyu na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne na wa tano.
No comments:
Post a Comment