Thursday, August 31, 2017

MUHIMBILI YAZINDUA MFUMO WA MALIPO KWA NJIA YA ELEKTRONIKI

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imefunga mashine 30 za ki-elektroniki katika maeneo ya kutolea huduma kwa lengo la kuimairisha na kudhibiti ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema mfumo huo utawezesha kuokoa zaidi ya Sh milioni 300.

Amesema Muhimbili imefunga mashine hizo kwa kushirikiana na Kampuni ya Maxcom na kwamba huduma hiyo itasaidia  kuokoa muda wa mgonjwa wakati wa kulipia huduma za matibabu.

“Muhimbili tunahudumia wagonjwa zaidi ya 2000 kwa siku, tulianza kudhibiti ukusanyaji wa mapato kwa kushirikiana na benki ya NMB tukaweza kuokoa takriban Sh milioni 300 lakini bado kuna baadhi ya malipo yalikuwa yakifanyika kwa ‘cash’.

“Kwa kuanzisha mfumo huu wa malipo ya kadi kwa kushirikiana na Maxcom kuanzia sasa hakuna malipo yatakayofanyika kwa ‘cash’,”.

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango Muhimbili, Gerald Jeremiah amesema mfumo huo umefanyiwa majaribio tangu Julai 10, mwaka huu hadi Agosti 15, mwaka huu na umeonesha mafanikio makubwa.

Mkururugenzi wa Kampuni ya Maxcom barani Afrika, Jameson Kasati alisema mteja ataweza kulipia huduma kwa njia mbalimbali.

“Mfumo huu unatumia njia mbili ambazo ni kadi na mfumo wa malipo kwa njia ya simu (mobile money), tumeanza na M-pesa, Airtel na Tigo baadae tutakwenda kwenye mitandao mingine,” alisema.

Amesema ili kuongeza mtaji wake, kampuni hiyo tayari imepeleka ombi katika Mamlaka ya Mitaji na Hisa ili waweze kununua hisa kwenye kampuni hiyo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment