Monday, August 7, 2017

Mbunge Stephen Ngonyani (Prof. Maji Marefu) Ataka Rais Magufuli aongezewe muda wa kukaa madarakani

Mbunge wa Korogwe Vijijini Steven Hillary Ngonyani alimaarufu kama Profesa 'Maji Marefu' amefunguka na kutaka Rais Magufuli aongezewe miaka mingine 10 ya kuongoza ili atawale nchi hii kwa miaka 20.

Majimarefu  amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa standi mpya ya mabasi iliyopo katika halmashauri ya mji wa Korogwe ambapo amedai kuwa Rais Magufuli anafanya kazi ambayo Watanzania wanaipenda na inaonekana hivyo itakuwa ni jambo jema kama ataongezewa muda zaidi ya kuongoza.

"Rais Magufuli wewe ni jembe sana na wewe umeletwa na Mungu katika watu ambao watasema katika halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambayo mimi ni mjumbe, basi mimi nitasema wewe uongezewe miaka hii miaka kumi haikutoshi, uongezewe miaka ufanye kazi miaka 20 na hilo pendekezo la Ilani ya uchaguzi lije mapema Mashekh wapo hapa, viongozi wa dini wapo hapa na sisi waganga wa kienyeji tupo hapa tutakuombea hilo wazo litapita, mtu anayefanya kazi hakuna kumbadilisha badilisha, unafanya kazi ambayo Watanzania wanaipenda tukibadilisha badilisha tunaweza kupata mtu ambaye ataimaliza nchi yetu" alisema Mbunge wa Korogwe Vijijini

Aidha Professa Majimarefu amesema kuwa wananchi wake wamekuwa wanyonge sana na kudai kuwa wao kama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wanashiondwa kusema baadhi ya mambo ambayo yanawarudisha nyuma kwa kuwa wanahofia kuchafua hali ya hewa.

"Rais tunaonewa sana na sisi hatupendi kusema hili kwa sababu ni viongozi wa CCM na serikali ya awamu ya tano haishikilii wabadhirifu, tumefanya mambo mengi Rais lakini kwa nguvu ya wananchi, leo wananchi wangu wanakuwa wanyonge kwa sababu hakuna mahali popote pakuwaletea maendeleo, maendeleo yanaletwa na wakulima, maendeleo yanaletwa na wafugaji lakini watu hawa wahawana maeneo ya kufanya maendeleo yao kwa kuwa maeneo yote yamechukuliwa na wawekezaji" alisisitiza Majimarefu.

Mbali na Profesa Majimarefu Rais wa Awamu ya pili nchini Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi amewahi kuzungumza na kutoa maoni yake kuwa kama isingekuwa Katiba ya Jumhuri wa Muungano wa Tanzania kuweka ukomo wa Rais kuongoza nchi basi Rais Magufuli angeongezewa muda wa kuongoza kwa kuwa amekuwa akifanya mambo mengi ambayo wao hawakuweza kufanya wakati wakitumikia nafasi hiyo ya Urais.

No comments:

Post a Comment