Meneja wa Mikopo wa TADB, Bw. Samuel Mshote akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu
Ndemanga (hayupo pichani) kuhusu fursa za mikopo inayotolewa na TADB.
Na mwandishi wetu, Lindi
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga ameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB) kuwasaidia katika kujenga na kuendeleza maghala ili kuwaweza wakulima wa manispaa hiyo kuhifadhi mazao yao.
Bw. Ndemanga amesema kuwa
maghala ya kuhifadhi mazao yamekuwa ni eneo lenye changamoto kubwa hali
inayorudisha nyuma tija kwa wakulima wa manispaa hiyo.
Akizungumza na ugeni kutoka TADB, uliongozwa na Meneja wa Mikopo wa Benki hiyo, Bw. Samuel
Mshote, Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza kuwa kutokuwa na maghala ya kutosha katika
manispaa kumekuwa kikwazo kikuu kwa wakulima kufikia malengo yao
kwa kuwa imekuwa ikiongoza gharama na upotevu mkubwa wa mazao yao.
“Changamoto ya uhaba wa maghala imesababisha manispaa kutokupata mapato stahiki kwa kuwa uhifadhi
wa mazao umekuwa ukifanyika katika maghala ya watu binafsi ambayo hayakidhi mahitaji halisi ya manispaa,” alisema Bw. Ndemanga.
Aliongeza kuwa ujio wa Benki ya Kilimo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto
hiyo.
Naye, Meneja wa Mikopo wa Benki hiyo, Bw. Samuel Mshote alisema kwa kutambua changamoto zinazowakabili
wakulima Benki ya Kilimo imeandaa mikopo maalumu kwa ajili ya kuendeleza
miundombinu ikiwemo ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao.
“Mikopo
hii ni kwa ajili ya kujengea miundombinu ya aina mbalimbali kwenye
mlolongo wa thamani, kwa mfano: skimu/ mifumo ya umwagiliaji, maghala ya
kisasa ya kuhifadhia mazao, pamoja na mahitaji mengine ya miundombinu
za kilimo,”alisema Bw. Mshote.
Kwa mujibu wa Bw. Mshote, mikopo ya aina hii itarejeshwa kwa awamu katika kipindi
cha miaka 5 hadi 15.
Akifafanua zaidi Bw. Mshote alisema kuwa ukokotoaji wa marejesho huendana na uwezo
wa kuilipa kwa kuzingatia mpango kazi, na hivyo kipindi kilichoridhiwa kwenye mkataba.
No comments:
Post a Comment