Kampuni
ya Lugumi Enterprises Ltd iliyotajwa katika sakata la zabuni ya Sh34
bilioni ya kuweka mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole
ya Jeshi la Polisi, iko hatarini kupoteza mali zake kutokana na kudaiwa
kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mnada
wa maghorofa hayo utafanywa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart,
kwa niaba ya TRA Mkoa wa Ilala. Maghorofa hayo yapo maeneo tofauti
jijini Dar es Salaam; moja Mtaa wa Mazengo, Upanga na mawili yako Mbweni
JKT wilayani Kinondoni.
Kuuzwa
kwa maghorofa hayo kumetangazwa jana katika gazeti la Serikali la
Sunday News, tangazo hilo likieleza kwamba ghorofa la Upanga linafaa kwa
ofisi wakati yale ya Mbweni JKT yanafaa kwa makazi.
Mkurugenzi
mtendaji wa Yono, Scolastica Kevela alisema mnada huo utafanyika
Septemba 9, kuanzia saa 4:30 asubuhi kwenye maeneo yalipo maghorofa
hayo.
Kevela alisema Lugumi Enterprises imeshindwa kulipa kodi ya TRA kwa wakati ndiyo maana wakapewa kazi ya kuuza majengo hayo.
Mkurugenzi huyo alikataa kutaja kiasi ambacho Lugumi anadaiwa na TRA pamoja na thamani ya maghorofa hayo.
Kevela alitoa rai kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Kwa
mujibu wa tangazo hilo, masharti ya mnada ni kulipa asilimia 25 ya
thamani ya bei kwa atakayefanikiwa kuyanunua maghorofa hayo.
Kiasi
kilichobaki kitatakiwa kulipwa ndani ya siku 14, tangu siku ya mnada na
kwamba atakayeshindwa kulipa katika kipindi hicho hatarudishiwa fedha
alizotoa na mnada utafanyika kwa mara nyingine.
Ukaguzi wa nyumba hizo unatakiwa kufanywa siku 10 kabla ya siku ya mnada.
Akizungumzia
hilo, mkurugenzi wa huduma na elimu ya mlipakodi wa TRA, Richard
Kayombo alisema Lugumi inadaiwa kodi za aina mbalimbali zinazotokana na
mapato yake.
Lugumi
ilikuwa gumzo mwaka jana baada ya taarifa ya CAG kuonyesha kuwa
ililipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha za zabuni kwa ajili ya kuweka
vifaa hivyo katika vituo 138, lakini hadi wakati wa ukaguzi ilikuwa
imeweka katika vituo 14 tu.
No comments:
Post a Comment