Na Francis Daudi,
Mysore +919513833624.
Mwezi wanne unaisha leo baada kumpumzisha mjomba ‘kathy’, shujaa wa ubaguzi wa rangi Afrika ambaye alifungwa katika gereza la Robben(pamoja na Nelson Mandela). Alikuwa ni maarufu hasa kutokana na tukio la Rivonia ambapo viongozi wa ANC akiwemo Walter Sisulu, Nelson Mandela, Andrew Mlangeni ,Denis Goldberg walikamatwa na kutumia kifungo cha muda mrefu.
Kama walivyo wanaharakati wengi, Kathrada alijiingiza katika vuguvugu la kupinga serikali ya kibaguzi huko Afrika kusini akiwa na miaka 12 tu, aliingia ‘Umoja wa Vijana wa kijamaa’ haitoshi alipofika miaka 17 alijiingiza kwenye chama cha South African Indian Congress. Katika umri huo aliongoza harakati za kupinga serikali na kutupwa jela mara kadhaa.
Miaka ya 1940 alifungwa kwa kosa la ‘Uhaini’ alikaa gerezani kwa muda kabla ya kupewa kifungo cha nyumbani. Huku akipigwa marufuku kushiriki shughuli zozote za kisiasa ikiwemo mikusanyiko ya kijamii. Aliendeleza vuguvugu chini chini na hatimaye alijiunga na Walter Sisulu na Nelson Mandela. Alipendwa sana na Mandela hasa kwa kuwa ndiye aliyekuwa msuka matukio ‘Mastermind’.
Akiwa na Mandela na Sisulu pamoja na wengine watano walikamatwa Julai 1963 na kisha kuhukumiwa mwaka 1964 katika kesi hiyo ya ‘Rivonia’. Kathrada alikuwa na miaka 35 tu, hivyo kuwa mfungwa mdogo zaidi katika kesi hiyo iliyotikisa dunia.
Kathrada alisoma na kutunukiwa shahada kadhaa kwa njia ya posta akiwa gerezani kama vile BA (History and Criminology) ‚ BA Bibliography (in African Politics and Library Science)‚ BA Honours (History) na BA Honours (African Politics-Siasa za Afrika). Aliachwa huru tarehe 15 octoba 1989. Hivyo, Kathrada alitumikia kifungo cha miaka 26 na miezi 3. Miaka 18 alikaa gereza lililopo kisiwa cha Robben. Aliporudi aliungana na mkewe Bi. Barbara Hogan ambaye pia alikuwa ameachiwa kutoka katika kesi ya uhaini.
Kathy ambaye pia aliitwa ‘Mjomba’ alichaguliwa kuwa mkuu idara ya uenezi na mawasiliano, wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 1994 bunge lilimchagua kuwa msaidizi wa raisi Mandela katika masuala ya bunge. Inaelezwa mara kadhaa alipata kutofautiana na Mandela.
Hasa suala la uchumi, yeye aliona ni lazima watu wa Afrika kusini waweze kuumiliki uchumi kupitia serikali yao ndipo uhuru utakuwa umekamilika. Aliona uhuru wa 1994 kama wa kisiasa na njia bora ya kuleta nafuu kwa wananchi ni kufuata siasa za kijamaa. Katika utangulizi wa kitabu chake ‘A Simple Freedom: The Strong Mind of Robben Island Prisoner‚ No. 468/64’ ulioandikwa na Mandela mwenyewe anamtaja Kathrada kama mtu mtambuzi, mwelevu na mwenye uwezo wa juu katika ‘mikakati’.
Hivi karibuni alikuwa mkali sana dhidi ya serikali ya Zuma, alimwandikia barua raisi Zuma kuwa ajiuzulu kama ameshindwa kuongoza. Haikushtua kwani Zuma anamfahamu vizuri Kathrada hasa misimamo yake. Pamoja na kuwa alikuwa kiongozi mpinga ubaguzi na kupata heshima kubwa Afrika lakini aliishi maisha ya kawaida kama wajamaa wengine.
Ameandika machapisho mengi na vitabu kama vile Letters from Robben Island (1999)‚ Memoirs (2004) and A Free Mind: Ahmed Kathrada’s Notebook from Robben Island (2005) na A Simple Freedom: The Strong Mind of Robben Island Prisoner‚ No. 468/64.
Kathy amefariki akiwa na umri wa miaka 87 katika hospitali kuu Johannesburg kwa tatizo la uvimbe mdogo katika ubongo. Wapo wanaodai ni kutokana na mateso na kazi za ‘sulubu’ alizopata gerezani. Mazishi yake yameudhuriwa na watu mbalimbali lakini rais Zuma hakufika ingawa alitangaza kama msiba wa kitaifa. Tukio la mazishi yake lilikuwa ni jukwaa la wanaharakati kukemea udhaifu na mwenendo mbaya wa serikali inayoongozwa na raisi Jacob Zuma.
Kama wanavyosema ‘shujaa uwa hafi’ hakika Kamaradi Ahmed Mohammed Kathrada ataendelea na harakati zake kupitia maandiko na mafundisho yake!
“Hatred‚ revenge‚ bitterness – these are negative emotions. The person harbouring those emotions suffers more.”- Ahmed Kathrada.
Imeandaliwa na Francis Daudi.
No comments:
Post a Comment