Rais John Magufuli akiakata utepe kufungua rasmi Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro eneo La Maweni Jijini Tanga.
Na Anna Makange, Tanga
RAIS John Magufuli amesema anamshangaa Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage kwa kuchelea kuwanyang'anya umiliki baadhi
ya wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda vilivyobinafsishwa na
serikali miaka 20 iliyopita na kusababisha matumizi ya maeneo hayo
kuhujumiwa.
Amemtaka waziri huyo kutoangalia sura au maamuzi yaliyopitishwa na
watangulizi wake, badala yake atumie sheria na kanuni zilizopitishwa,
kuhakikisha anavifutia usajili viwanda vyote vilivyobinafsishwa na
kushindwa kuendeleza uzalishaji kwa muda mrefu sasa ambavyo vimegeuka
kuwa maficho ya wanyamapori.
Dk Magufuli alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi
katika Kata ya Maweni jijini Tanga wakati wa sherehe za kuweka jiwe la
ufunguzi wa kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro. Kiwanda cha saruji cha
Kilimanjaro kinachozalisha saruji ya kiwango cha 32.5N na 42.5N, ujenzi
wake ulianza mwaka 2013 kinatarajiwa kuzalisha tani 3,000 kwa siku,
ambapo kwa sasa uzalishaji ni tani 800 na kimejiari wafanyakazi 189.
“Hivi wewe waziri mwenye dhamana kwa nini kila wakati nasikia na
kuona viwanda mbalimbali vikifunguliwa, lakini nashangaa kwa sababu
sijasikia viwanda visivyozalisha vikifutwa kama anavyofanya mwenzako wa
Wizara ya Ardhi kufuta hati za umiliki wa ardhi za mashamba mkubwa? Sasa
nakuomba kwa mara ya mwisho hebu fumba macho na uwakung'ute,” alisema
Dk Magufuli na kuongeza: “Mimi ndiye niliyekuteua kushika dhamana hii ya
viwanda na biashara, sasa unaogopa nini? Kuanzia sasa nataka nisikie
watu wamenyang'anywa, hatuwezi kuendelea kuacha maeneo hayo ya wananchi
ambayo watu wameuziwa kwa bei mdogo na kuyatelekeza “Nenda kawatoe,
usijali hata kama mmiliki ni kutoka CCM wewe nyang'anya, ikiwa ni
mwanachama wa CUF, Chadema awe ni waziri au mbunge wewe nyang'anya.
Hawatakufanya jambo lolote hatuwezi kuendelea kuruhusu jambo hili
liendelee.” Alifafanua, “Nchi hii imechezewa sana, viwanda hivi vilikuwa
ni mali ya Watanzania na wenzetu waliovinunua wameamua kuviua. Kwa
mfano, hapa Tanga kwenye taarifa yenu hapa imeeleza kwamba kuna viwanda
kumi na mbili vilivyobinafsishwa vyote havifanyi kazi, sasa wakati
umefika kwamba lazima viwanda virejeshwe serikalini ili wakuu wa mikoa
wakabidhi wawekezaji wengine wanaohitaji kufanya uzalishaji.”
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, nchi nzima ina viwanda 197
vilivyotelekezwa baada ya kubinafsishwa takribani miaka 20 iliyopita,
vikiwemo viwanda vilivyopo mkoani Tanga. Aidha, Rais Magufuli aliwaagiza
wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanatembelea na kufanya tathmini
ya viwanda vyote vya serikali vilivyoko katika maeneo yao, ambayo kwa
sasa havifanyi uzalishaji na kuwasilisha orodha na mapendekezo ya
kuvifuta ili waziri aweze kuwanyang'anya wamiliki.
Akizungumzia kiwanda hicho cha saruji cha Kilimanjaro
kitakachozalisha tani 3,000 kwa siku baada ya ujenzi kukamilika,
aliwapongeza wawekezaji hao kwa kutoa huduma kwa jamii na kumwagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuingiza kwenye
mpango wa halmashauri barabara yenye urefu wa kilometa 3.5 inayoingia
kiwandani hapo ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za ukarabati.
“Kwa kuwa hawa ni wawekezaji wazalendo, hawadaiwi kodi na wameweza
kutia mifuko 1,300 ya saruji kusaidia ujenzi wa zahanati, madarasa
katika kata hii ya Maweni, basi nami nakuagiza mkurugenzi hii barabara
iweke kwenye mipango ya halmashauri kwa kutumia bajeti ya mfuko wa
barabara ili kiwanda kitumie fedha hizo kuongeza mishahara ya
wafanyakazi,” alieleza Dk Magufuli.
Tanzania kwa sasa ina jumla ya viwanda 11 vyenye uwezo wa kuzalisha
tani milioni 10 za saruji kwa mwaka, wakati mahitaji ya sasa ya bidhaa
hiyo ni wastani wa tani milioni 4.7. Baada ya kufungua kiwanda cha
saruji cha Kilimanjaro, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la upanuzi
wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga (Tanga Fresh), ambacho
kinatarajia kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 50,000 kwa siku
hadi kufikia lita 120,000, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya
wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya wafugaji 24 kwa
asilimia 42 na mwekezaji kutoka Uholanzi kwa asilimia 58 na upanuzi
unaofanywa, utaongeza uwekezaji kutoka Sh bilioni 12 hadi kufikia Sh
bilioni 26.5. Akiwa kiwandani hapo, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kukabidhi hati miliki ya kiwanda hicho kwa
menejimenti ya kiwanda, na ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
iliyokuwa ikidai kodi ya ongezeko la mtaji kuelekeza madai hayo kwa
mmiliki wa awali wa kiwanda hicho, aliyewauzia wakulima.
Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage kuchukua hatua dhidi ya kiwanda cha maziwa cha Arusha
ambacho baada ya kubinafsishwa, kimegeuzwa kuwa kituo cha kukusanyia
maziwa na kuyasafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kusindikwa. Pia
amemwagiza Mwijage kuwa nchi yoyote itakayozuia maziwa ya Tanzania, nayo
izuiwe kuingiza maziwa yake nchini.
Aidha, ametoa siku tano kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk
Charles Tizeba kufika kiwandani hapo na kushughulikia changamoto
zinazokikabili kiwanda hicho. Rais Magufuli pia amefungua awamu ya
kwanza ya mradi wa kituo cha matangi ya mafuta cha GBP kilichopo katika
eneo la Raskazone, Tanga ambacho kina uwezo wa kuhifadhi lita milioni
122.6 na ambacho kinatarajia kupanuliwa hadi kufikia lita milioni 300
ifikapo katikati ya mwaka ujao.
Dk Magufuli alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa GBP, Badar Sood kwa
uwekezaji huo mkubwa wa Sh bilioni 60 utakaojumuisha ujenzi wa kiwanda
cha vilainishi na kiwanda cha kusindika gesi na amemhakikishia kuwa
serikali itaendelea kumuunga mkono wakati wowote. Pia Rais Magufuli
alimpongeza Sood kwa kulipa kodi ipasavyo, ambapo katika miaka miwili
iliyopita ameongeza malipo ya kodi kutoka Sh bilioni 208.950 hadi
kufikia Sh bilioni 293.263 na aliwahakikishia wawekezaji wote wanaolipa
kodi ipasavyo kuwa wapo salama na serikali itawalinda. Rais Magufuli
alielezea kutoridhishwa kwake na kusuasua kwa mchakato wa ununuzi wa
mita za kupimia mafuta, yanayoshushwa kutoka melini.
No comments:
Post a Comment