Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imedhamiria kuvipa kipaumbele katika ugawaji wa mikopo vikundi vitakavyotoka katika kaya masikini
Hayo yamesemwa na mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wilayani humo ndugu Kagwe Samson wakati akizungumza na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini wanaoishi kata ya Kayenze kabla ya kuanza kwa zoezi la uhawilishaji wa fedha kwa kaya hizo masikini ambapo amewataka wananchi hao mbali na kutumia vizuri fedha hizo kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ili waweze kujikwamua kutoka katika umasikini kuhakikisha wanajiunga katika vikundi vya shughuli za uzalishaji na kuweze kukopesheka
‘… Serikali kupitia halmashauri yenu ya manispaa Ilemela haina uwezo wa kusaidia mtu mmoja mmoja hivyo mnatakiwa kujiunga katika vikundi kulingana na shughuli mnazozifanya kama biashara ndogo ndogo, kilimo, uvuvi mwisho wa siku halmashauri iweze kuwasaidia na halmashauri itaisaidia vile vikundi vilivyo imara vimesimama, Manispaa imeahidi kuvipa kipaumbele vikundi vilivyotoka katika kaya masikini kwa maana ya Tasaf katika ugawaji wa mikopo…’ Alisema
Kwa upande wake akitekeleza zoezi hilo la uhawilishaji fedha kwa walengwa hao ndugu Frank Ngitaoh ameongeza kuwa kwa awamu hii ya tatu mzunguko wa kumi na tatu jumla ya shilingi milioni mia moja arobaini na elfu kumi na mbili zimetengwa kuzifikia kaya elfu tatu mia tisa na arobaini na nne kwa mitaa mbalimbali ya kata za wilaya ya Ilemela isipokuwa mitaa ya kata ya Kahama ambayo haipo kwenye mpango kwa awamu hii ili kusaidia kaya hizo masikini katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi
Aidha zoezi hilo limeenda sambamba na utoaji wa elimu kwa walengwa juu ya namna bora ya matumizi ya fedha hizo sanjari na elimu ya uundwaji wa vikundi vya ujasiriamali vya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi kujikwamua kutoka katika lindi la umasikini
Akihitimisha mwenyekiti wa mtaa Kayenze Robert Galula mbali na kuishukuru Serikali kwa uendeshaji wa zoezi hilo amewataka viongozi wenzake kushirikiana kwa pamoja katika kusaidia kutatua changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza sambamba na kusimamia haki na usawa kwa walengwa
No comments:
Post a Comment