Friday, August 18, 2017

IKUNGI KUTOKOMEZA UKEKETAJI, MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Mhe.Miraji Mtaturu (aliyesimama) amezindua mradi wa AWARE unaosimamiwa na Shirika la Stars of Power Rescue Foundation SPRF, la mkoani humo unaolenga kufanya utetezi wa haki za watoto na wanawake dhidi ya mila na desturi kandamizi katika jamii.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika jana, Mhe.Mtaturu aliwahimiza wasimamizi wa mradi huo kujikita zaidi kwenye kutoa elimu katika jamii ili kuondokana na mila kandamizi.

Aidha aliwataka wazazi na walezi kutowabagua watoto wao bali wawalee katika misingi ya usawa kwa kutoa haki sawa kwa watoto wote, wa kike na wa kiume ikiwemo haki sawa ya kupata elimu, kwani kuna baadhi ya wazazi bado wanaamini watoto wa kike ni kwa ajili ya kuolewa na wa kiume ni kwa ajili kurithi mali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bi.Rustika Turuka, aliwahimiza watendaji kuutumia vyema mradi huo katika kuongera ari zaidi kwa wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo na uongozi.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la SPRF, Dr.Suleiman Mutani alisema mradi wa AWARE umefadhiriwa na shirika la The Foundation For Civil Society kwa kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi huu, ukilenga kuongeza uelewa katika jamii ili kuondokana na vitendo vya ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni.
Mkurugenzi wa Shirika la SPRF, Dr.Suleiman Mutani akizungumza kwenye uzinduzi huo. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Ikungi anayefuata ni Katibu Tawala wilayani humo na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa polisi wilayani Ikungi.
Watendaji mbalimbali wa shirika la SPRF (waliosimama), wakijitambulisha kwenye uzinduzi huo
Watendaji mbalimbali wilayani Ikungi
BMG Habari

No comments:

Post a Comment