Saturday, August 12, 2017

DOKTA MPANGO AWASIMAMISHAKAZI WATUMISHI 4 WA TRA MPAKANI TUNDUMA

Image result for dr philip mpango

Na Benny Mwaipaja, Songwe/Mbeya

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewasimamisha kazi watumishi wanne wa Idara ya Forodha, katika Mpaka wa Tanzania na Zambia, Mjini Tunduma, ili kupisha uchunguzi wa kudaiwa kuhusika na upotevu wa lakiri 10 zinazotumika kufunga kwenye shehena ya mizigo inayopita mpakati hapo kutoka nje ya nchi. 
Mpango amewataja watumishi hao kuwa ni pamoja na Harrison Mwampashi, John Makorere, Stephene Josia na Frank Kessy na kuviagiza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama mpakani hapo viwahoji huku wakiwa wamesimamishwa kazi.

Watumishi hao wanadaiwa kuiba lakiri hizo kumi kutoka ofisi za TRA-Tunduma wanakofanyiakazi, ambapo 4 kati ya hizo lakiri zilikutwa zimefungwa kwenye mizigo ya malori yanayoshikiliwa katika mpaka huo baada ya uchunguzi kufanyika huku malori mengine 5 yakizuiwa baada ya kuonekana lakiri zao zimechezewa.

Taarifa zinasema kuwa baada ya uchunguzi, mawakala ama wamiliki wa malori hayo wamedai walipewa lakiri hizo na watuhumiwa na kwamba uchunguzi zaidi umebaini kuwa kiwango cha mizigo kilichomo kwenye makontena yaliyobeba mizigo ya magogo na kufungwa lakiri hizo za wizi hakilingani na idadi ya mizigo iliyoko kwenye nyaraka jambo linaloashiria kuwa wanazitumia lakiri hizo kudanganya idadi na uzito wa mizigo yao ili kukwepa ushuru na kodi mbalimbali za Serikali.

“Hakuna kitu muhimu kama uadilifu kwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato na hatutasita wala hatutamwonei aibu mtu yeyote, tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria ili kulinda fedha za umma” alionya Dkt. Mpango

Alisema kuwa Serikali imebaini baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato na Idara za Forodha mipakani wanashirikiana na wafanyabishara wasio waaminifu kuingilia mifumo ya kukusanyia mapato, kitendo ambacho kinaweza kurudisha nyuma juhudi za serikali kuwahudumia wananchi wake.

Dkt. Mpango amewaonya wafanyakazi wote wa forodha na Mamlaka ya Mapato nchini, kuwa wazalendo na waaminifu katika kukusanya mapato ya Serikali na kuacha kujihusisha na vitendo vinavyokwaza ufanisi wa Mamlaka hayo.

BIASHARA YA KUBADILISHA FEDHA MPAKANI

Wakati huo huo, Dkt. Mpango, ametoa muda wa siku thelathini, kwa wanaobadilisha fedha za kigeni kiholela mipakani, waache mara moja, badala yake waheshimu sheria za Nchi, na kuunda vikundi vinavyoweza kuanzisha maduka ya kubadilisha fedha hizo.

Alitoa kauli hiyo Mjini Tunduma, wakati akizungumza na wabadilisha fedha mpakani humo, kwamba serikali itawaheshimu tu wale watakaojiundia vikundi na kuwa na sehemu wanakoweza kubadilisha fedha kwa kufuata utaratibu na wala si vinginevyo.

ATEMBELEA UJENZI WA KITUO KIPYA CHA FORODHA NA IDARA YA FORODHA TUNDUMA

Akiwa Mjini Tunduma, Dkt. Mpango, pamoja na mambo mengine ametembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha pamoja cha Forodha cha Mpaka kati ya Tanzania na Zambia Mjini Tunduma.

Pia ametembela Ofisi ya Idara ya Forodha mpakani hapa, na kupata taarifa ya makusanyo ya mapato kwa mwaka wa Fedha wa 2016/2017, ambapo maafisa wamekusanya mapato zaidi ya Bilioni 75 na kuvuka lengo la mapato waliyokuwa wameyatarajia.

Meneja wa Idara ya Forodha mikoa ya Mbeya na Songwe, Bw. Jimmy Nsindo amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo, Mpaka huo wa Tanzania na Zambia, ni mpaka unaoweza kuingilika kirahisi, matokeo yake udhibiti wa mapato unaingia dosari, huku baadhi ya watanzania wanafanya biashara zinazodaiwa kuliingizia hasara taifa, zikiwemo za kubadili fedha za kigeni kwa mfumo usio rasmi.

ASHITUKIZA VITUO VYA MAFUTA

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametoa muda wa siku ishirini kwa wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao wameomba kupatiwa mashine za Kielectroniki kwaajili ya kuunganishwa na mfumo wa kodi na utoaji wa risti wawe wamepata mashine hizo vinginevyo watafungiwa vituo vyao.

Aidha, amesema ifikapo Jumatano Juma lijalo wamiliki wote wa maduka mkoani Mbeya, waanze kutumia mashine za Kielekroniki za kutolea risiti (EFDs) na kuonya kwamba Serikali haitasita kuyafunga maduka yao wasipotekeleza maagizo hayo.

Waziri wa Fedha na Mipango ametumia ziara hii kutoa shukrani kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya namna walivyoitikia kulipa kodi za nyumba.

No comments:

Post a Comment