Na Halima Mlacha
SERIKALI iko katika mchakato wa kumalizia ramani za mipango miji yote
nchini, huku baadhi ya miji, ikiwemo Mwanza, Arusha, Mtwara, Singida na
Iringa ramani zake zikiwa zimekamilika.
Pamoja na hayo, pia imeanza mkakati wa kupiga picha za anga katika
wilaya zote nchini na tayari wameanza na Jiji la Dar es Salaam, na picha
hizo zitatumika kwa ajili ya kupanga miji na kutengeneza ramani ya
msingi inayoonyesha hali halisi ya nchi.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Kaimu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses
Kusiluka, katika mahojiano maalum aliyoyafanya na magazeti ya serikali
Daily News na HabariLeo.
Alisema serikali ililazimika kuandaa ramani mpya za mipango miji
baada ya ramani nyingi zilizopo kupitwa na wakati na hali ya majiji
mengi kutopangika ipasavyo. Alisema katika mchakato huo, alitaja miji
ambayo bado ramani zake ziko katika hatua ya mwisho kuwa ni pamoja na
jiji la Dar es Salaam na Dodoma, ambayo ililazimika ramani zake
kuboreshwa zaidi kutokana na mkoa huo kuwa makao makuu ya serikali.
“Master Plan nyingi kwa ukweli zimekamilika, zipo chache zinaendelea
katika hatua ya mwisho na zikikamilika, tunatarajia kufanya uzinduzi wa
ramani hizo ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo, na kupitia picha hizi
sasa ramani zote na matumizi ya ardhi zitaandaliwa kieletroniki,”
alisisitiza.
Akizungumzia picha za anga, alisema picha hizo ni muhimu kwa
maendeleo ya Tanzania kwani pamoja na kutumika katika mipango ya
matumizi ya ardhi, pia zitatumika kwa ajili ya kupanga miundombinu,
majanga na mipango miji. Kwa upande wa upimaji viwanja, Dk Kasiluka
alisema wizara hiyo ina mpango wa kuhakikisha maeneo yote nchini
yanapimwa na wamiliki wa ardhi kupatiwa hati au hati za kimila.
No comments:
Post a Comment