Friday, July 14, 2017

Waziri Mkuu Atembelea Mradi Wa Kusafirisha Umeme Lindi.......Asema changamoto ya kukatika umeme Mkoa wa Lindi kuwa historia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema changamoto ya kukatika umeme katika mkoa wa Lindi kuwa historia baada ya kukamilika kwa mradi wa kusafirisha umeme wa kilovolti 132 Mtwara-Lindi.

Amesema hayo  jana (Alhamisi, Julai 13, 2017) alipotembelea mradi huo wa kuzalisha umeme unaojengwa katika kijiji cha Mahumbika wilayani Lindi.

Waziri Mkuu alisema kukamilika kwa mradi huo uliogharimu sh. bilioni 16 kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Lindi.

Alisema mkakati wa Serikali ni kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme ili Watanzania wapate umeme mwingi utakaosambazwa hadi vijijini kwa gharama nafuu.

“Mikoa wa Lindi ulikuwa na shida kubwa ya kukatika kwa umeme, kukamilika kwa mradi huu ni mkombozi kwetu, tunawakaribisha wawekezaji waje kuwekeza kwa sababu sasa tunanishati ya uhakika.”

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe alisema kuimarika kwa upatikanaji wa umeme kutawezesha safari ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

 Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema atahakikisha anapambana na watu wote watakaokwamisha jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuwahudumia wananchi.

 Pia ameahidi kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi wote Tanzania bila ya kujali maeneo wanakotoka wala itikadi zao za kisiasa na kidini.

 Ameyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Nanganga, Nyangao, Mtama na Nyengedi alipowasilisi wilayani Lindi, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

  “Tunataka fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwahudumia wananchi zitumike ipasavyo na hatutakubali kuona mtu napewa fedha na kuzitumia atakavyo.”

 Pia Waziri Mkuu amewataka wananchi hao kuweka pembeni  itikadi zao za kisiasa na badala yake washirikiane kwa pamoja katika kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao.

 “Rais Dkt. Magufuli amesema Watanzania kwa sasa hatuhitaji kufanya siasa, sasa ni kazi tu, hivyo tutumie muda wetu mwingi kwa kufanya kazi za maendeleo. Tupunguze muda wa kubishana hakuna tija watu wanataka maji, afya.”

 Awali Mbunge wa jimbo la Mtama Mheshimiwa Nape Nnauye kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo aliishukuru Serikali kwa kuboresha huduma mbalimbali kwenye jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment