Friday, July 14, 2017

Makamu wa Rais: Hatupo Tayari Kupokea Misaada ya Wafadhili Wenye Mashart ya Kudhalilisha Utu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema Taifa halipo tayari hata kidogo kupokea misaada kutoka kwa wafadhili wenye masharti ambayo hayaendani na mila na desturi za kitanzania.

Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Ireland Mary Robinson pamoja na mwanzilishi wa Taasisi ya Graca Machel, Craca Machel pamoja na ujumbe walioambatana nao Ikulu- Jijini Dar es Salaam.

"Kuna baadhi ya wafadhili wanaisaidia serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na bajeti vizuri sana na bila masharti mabaya lakini kuna baadhi ya wafadhili wanaonyesha wazi kuwa wanataka serikali ikubali masharti yao ambayo yanaenda kinyume na maadili ya taifa kitu ambacho hakiwezekani" amesema Mhe. Samia.

Pamoja na hayo, Mhe Samia Suluhu amesema kuwa serikali imeongeza maradufu bajeti yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa viwango vinavyotakiwa nchini.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Ireland Mary Robinson pamoja na mwanzilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Graca Machel, Craca Machel wameipongeza serikali kwa jitihada inazozifanya katika uimarishaji wa sekta ya afya nchini na wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha huduma za afya nchini zinaendelea kuboreshwa ipasavyo.

No comments:

Post a Comment