Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT imefanya kikao chake cha Kikatiba tarehe 18/07/2017, ambapo pamoja na mambo mengine ilijadili agenda mbalimbali za msingi kuhusu uchaguzi ndani ya Jumuiya. Pia wamejadili juu ya hali ya amani na usalama, uchumi na maendeleo ya Jamii ambapo Kamati imeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mafanikio makubwa ya bajeti ya mwaka 2016/2017, na pia mipango mikubwa ya maendeleo iliyoainishwa kwenye bajeti ya 2017/2018.
KUHUSU UCHAGUZI WA UWT;
Uchaguzi kwa ngazi ya Matawi umefanyika kwa asilimia 95, ngazi ya Kata vikao vya uchujaji vinaendelea na kwa ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa uchaguzi unaendelea, tarehe 02 – 10/07/2017 wanachama walijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, kujitokeza kwao kwa wingi kumethibitisha imani yao kubwa kwa Jumuiya na Chama Cha Mapinduzi. Kwa nafasi ya Mwenyekiti wa UWT waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ni wanachama 34, nafasi ya Makamu Mwenyekiti wanachama walijotokeza ni 14, wajumbe wa NEC bara 33 Baraza Kuu ni 73 wakilishi Vijana 15na Wazazi 15 Kwa upande wa Zanzibar wajumbe wa NEC 13 wajumbe wa Baraza Kuu ni 40. Jumla ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa jumla yao ni 7,643
Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT imewapongeza wanachama wote waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea. Pia, inatoa wito kwa wanachama wote kuendelea kuzingatia Kanuni za Uchaguzi na Maadili kwa kutotangaza nia, kutounda makundi na safu za kampeni pamoja na kujizuia kutoa na kupokea rushwa. UWT inasisitiza kuwa, RUSHWA ni adui wa HAKI. Tutakuwa Jumuiya ya mfano,kwani hatutamvumilia yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa.
UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI;
Kwa namna ya kipekee UWT inaipongeza Serikali kwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM wenye mafanikio makubwa wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu makusanyo ya ndani yamefikia takribani Shs. trilion 14.4, makusanyo hayo yakienda sambamba na ukuaji wa uchumi kwa asilimia 7.0% na kupungua kwa mfumuko wa bei kutoka 6.5% hadi kufikia 5.4%.
UWT itanatambua heshima kubwa ambayo nchi yetu imeipata kutoka kwa mataifa ya Afrika na kote duniani kwa kazi kubwa wanayoifanya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Mhe. Rais Dkt. Ali Mohamed Shein ya kurudisha nidhamu ya matumizi Serikali na mapambano yao dhidi ya rushwa.
Kwa msisitizo mkubwa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT imepongeza ununuzi wa ndege mpya, uamuzi wa kutoa elimu bure na mikopo ya elimu ya juu, hatua ambayo imewakomboa familia za kipato cha chini na watoto wenye hali duni kuendelea na masomo yao na kujikomboa kutoka katika hali ya umasikini. Pia, tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kuunda mamlaka ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar (ZPRA) na ongezeko la mishahara kwa asilimia 100 kwa wafanyakazi Serikalini.
UWT inatia shime utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege, barabara za juu (flyovers), ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge, ununuzi wa vivuko, meli na ujenzi wa madaraja makubwa.
Wanawake nchini kote tumepata faraja kubwa kwa hatua ya Serikali kuondoa ushuru, kodi na tozo za kero kwenye mazao na biashara ndogo ndogo, kupanda kwa bei ya mazao ya biasharakama vile Korosho na Pamba kumewakomboa wanawake wakulima vijijini. UWT inaitaka Serikali kuhakikisha Halmashauri zote zinatenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake na vijana pamoja na kupeleka milioni 50 kwa kila kijiji ili zitumike kutoa mikopo kwa wajasiriamali na uimarishaji wa benki ya wanawake. Usambazaji wa huduma za maji na umeme vijijini kumeendelea kuondoa uzito mkubwa uliokuwa unawakabili wanawake vijijini wa kutafuta maji kutoka umbali mrefu, pamoja na mafanikio hayo tunaitaka Serikali kuongeza juhudi katika usambazaji wa maji hasa katika maeneo ya vijijini.
UWT inaungana na wanawake wote kuishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za Afya na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano (5), ununuzi wa mashine na vifaa tiba ikiwemo usambazaji wa dawa na vitanda hospitalini, vituo vya afya na zahanati.Kama ilivyotajwa kwenye ilani ya CCM ya 2015/2020, UWT tunasisitiza na kuitaka Serikali kutimiza lengo la kuwa na Zahanati katika kila kijiji, Kituo cha Afya kila Kata na Hospitali kila Wilaya, jambo hili liende sambamba na ujenzi wa maghala ya kisasa ya Bohari ya Dawa (MSD) mikoani.
Aidha, Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) imeridhishwa na mwelekeo na kasi ya serikali kufikia uchumi wa viwanda, hatua za ujenzi na uzinduzi wa viwanda mbalimbali nchini kote. Mabadiliko ya sera na sheria ya uchimbaji wa madini, mafuta na gesi yanatoa faraja na matumaini makubwa kwa Watanzania hasa wanawake kuelekea uchumi wa kati.
HALI YA AMANI NA USALAMA;
Katika hatua nyingine UWT inaiunga mkono Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua mbalimbali wanazochukua kukabiliana na hali ya uvunjifu wa amani na mauaji yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini kama vile Kibiti, Rufiji na Mkuranga. Unyama uliofanywa hauvumiliki kwani umesababisha wanawake wengi kubaki wajane wakihangaika na ulezi wa watoto na familia zao. Tunatoa wito kwa wanawake, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi kuungana pamoja kukemea na kumuomba Mwenyezi Mungu kutuondolea janga hili.Tunasisitiza Serikali kuongeza nguvu zaidi ili kumaliza kabisa matukio hayo.
Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) tumesikitishwa sana natunalaani vikali kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa zenye viashiria vya kuchochea uvunjifu wa amani na umoja wa kitaifa. Nchi yetu Mwenyezi Mungu ameibariki sana, ni nchi ya umoja, amani, upendo, heshima na mshikamano. Kauli hizo zinazotolewa zinavunja heshima ya viongozi wakuu wa nchi, heshima ya Serikali na Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunatoa wito kwa wanawake wenzetu na wananchi kutounga mkono, kujitenga na kuzipinga kauli hizo zisizo na staha kwa viongozi, zinazolenga kuleta mfarakano katika jamii yetu.
Aidha, tunatoa msisitizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaotoa kauli zenye viashiria vya wazi vya kuchonganisha Watanzania na kuvuruga amani ya nchi. Serikali iendelee kukemea na kuchukua hatua bila kuhofia hadhi, cheo ama sura ya mtu ili mradi amevunja sheria za nchi.
UWT tunaendelea kuhimiza wanawake na watanzania kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kujikomboa na umasikini na kuchangia maendeleo ya nchi. Wanawake na vijana ndio nguvu kazi inayotegemewa kuliendeleza Taifa.
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) tumepokea kwa furaha kubwa taarifa ya matokeo ya kidato cha sita mwaka 2017, yaliyoonesha watoto wa kike kuongoza kufanya vizuri katika mitihaniyao. Tunawapongeza na kuwasisitiza watoto wa kike kuongeza juhudi na kujituma zaidi ili waendelee kufanya vizuri kwani wanao uwezo wa kufanya vizuri zaidi.
UWT tunatoa wito kwa wanawake na wananchi wote, kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kujituma na kufanya kazi. Tufanye KILA LINALOWEZEKANA kulinda, kuimarisha Utaifa na Umoja wetu. Tulinde heshima za viongozi wetu na kujiepusha na kauli, matendo na mipango yenye kulenga kudhohofisha Utanzania wetu.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na:
Amina Nassor Makillagi (MNEC, MB)
KATIBU MKUU WA UWT
19/07/2017
No comments:
Post a Comment