Serikali
Mkoani Simiyu imejipanga kuweka mkakati
maalum utakaowasaidia wafugaji mkoani humo kutoka kwenye ufugaji wa kuhama hama
na kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija.
Hayo
yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika kikao maalum
cha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji, wataalam na wadau mbalimbali
wa mifugo kutoka ndani na nje ya mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa
Katoliki mjini Bariadi.
Mtaka amesema Mkoa wake umedhamiria
kuwatambua wafugaji na maeneo yao na kutoa elimu juu ya upimaji wa maeneo hayo ili
yatumiwe kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhama hama kufuata maji na malisho
katika mikoa mingine.
“Hatuwezi kuwa Serikali ambayo
ina majibu mepesi kwenye mambo ya msingi, lazima tupate majawabu ya wafugaji
ndani ya mkoa wetu, tufike mahali ambapo mfugaji kutoka mkoa wa Simiyu
hatapigwa faini kwenye mikoa mingine kwa sababu ya kutafuta maji na
malisho”amesema Mtaka.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema
Serikali kupitia Wataalam wa Kilimo na Mifugo watatoa elimu kwa Wafugaji
watakaorasimisha maeneo yao, ili wayatumie kupata malisho ya mifugo na kuweka
miundombinu muhimu ya mifugo kama vile malambo, majosho na visima katika kukabiliana
na changamoto ya upungufu wa maji na malisho ya mifugo.
Ameongeza kuwa, Mkoa unaandaa
utaratibu ambapo shule za Serikali zitakapokuwa zinafungwa, Idara ya Kilimo na
Mifugo itatumia madarasa hayo kutoa elimu ya ufugaji na kilimo bora kwa wananchi.
Sanjali na hilo, Mkuu huyo wa
Mkoa amesema zoezi la kupima maeneo ya wafugaji na kuweka miundombinu muhimu ya
mifugo litakapokamilika Serikali imepanga kuweka mizani katika minada yote
mkoani humo ili wafugaji wasidanganywe na kuibiwa wanapouza mifugo yao.
Kwa upande wake Padre John
Kasembo ambaye ni Mwezeshaji na Mshauri katika Masuala ya Uongozi, Ujasiriamali
na Maendeleo ametoa wito kwa Wafugaji wa
Mkoa wa Simiyu kukubali kufanya ufugaji wenye tija na waungane na Viongozi
katika mipango inayoandaliwa kwa ajili ya kufikia ufugaji bora kwa manufaa yao.
Padre Kasembo amesema ili
wafugaji wafuge kisasa wanapaswa kuwa na maeneo, miundombinu ya kisasa, malisho
na kufuata sheria na taratibu, hivyo akawaasa wakubali kubadilika katika namna
ya kufikiri, kutenda, kuweka vipaumbele na kushughulikia changamoto ili wapate
matokeo chanya.
Daktari wa Mifugo wa Sekretarieti
ya Mkoa wa Simiyu, Gamitwe Mahaza amesema Wafugaji wengi pia ni Wakulima, hivyo
ni vema wakatumia masalia ya mazao kwa ajili ya malisho badala ya kuyaacha
mashambani yakaharibika; akasisitiza juu ya urasimishaji wa maeneo yao ili
miundombinu kama visima iwekwe kusaidia ukuaji wa malisho ya asili na upandaji
wa malisho ya kisasa.
Naye Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA
kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC), Mhandisi George Mulamula
ameeleza kuwa upimaji katika maeneo ya wafugaji unaweza kufanyika kwa kutumia
njia mbalimbali zikiwemo zinazotumia mifumo ya TEHAMA , kama vile matumizi ya satelite
na ndege zisizotumia rubani (drones)
ambazo zitasaidia zoezi hilo kufanyika kwa usahihi mkubwa na haraka.
Pia Mhandisi Mulamula amesema
kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wafugaji wataweza kupata
mafunzo na taarifa mbalimbali za mifugo kupitia simu zao za mikononi, kujua bei
na soko la mifugo na kutambua mifugo yao hivyo kupunguza wizi wa mifugo.
Viongozi wa Wafugaji na Wafugaji
kwa pamoja wameshukuru Uongozi wa Mkoa kuona umuhimu wa kushughulikia
changamoto zao ambapo wamesema kwa kuwa wana maeneo ambayo hayajapimwa
wameiomba Serikali kupitia Idara ya Ardhi kupima maeneo hayo na Idara ya Mifugo
iendelee kutoa elimu ya ufugaji bora.
“Tunaushukuru sana uongozi wa Mkoa
kwa kuliona hili, mimi naomba maeneo yetu yapimwe na sisi wafugaji tuelimishwe
kufuga kisasa, wafugaji wengi tuna maeneo ila ng’ombe tumewapeleka mikoa
mingine kwa sababu hatujui tunayatumiaje maeneo yetu, wataalam watuelimishe
namna ya kuyatumia” amesema Yohana Mnyumba, Mfugaji kutoka Wilaya ya Bariadi.
No comments:
Post a Comment