Sunday, July 30, 2017

SHAKA AHITIMISHA ZIARA YA KUKAGUA UTEKEKEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI KATIKA MKOA WA KIGOMA NA MWANZA

Na Mathias Canal, Mwanza

Ziara ya Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka (MNEC) ya Siku 14 kwa kuzuru katika Wilaya 13, Saba zikiwa za Mkoa wa Kigoma na Wilaya 6 zikiwa za Mkoa wa Mwanza imefikia ukomo juzi Julai 27, 2017 katika Wilaya ya Sengerema huku ikiwa imevuna wanachama wapya zaidi ya 100.

Katika Ziara hiyo Shaka alijikita zaidi katika kusikiliza Changamoto Mbalimbali zinazowakabili Vijana zihusuzo Jumuiya ya vijana na zile zinazohusu Serikali moja kwa moja ikiwemo kutotolewa mikopo ya asilimia 5 kama kusudio la utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 iliyoielekeza Serikali kutenga mikopo hiyo kwa makundi ya vijana na Wanawake.

Shaka alibaini kuwa kasi ya Halmashauri nchini katika utoaji mikopo bado ni ndogo sana kwani katika Halmashauri hizo 13 ni Halmashauri 4 pekee ndizo zinazofanya vizuri katika utoaji mikopo.

Vijana Mbalimbali nchini wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi na wale wanaotokana na vyama vingine visivyokuwa CCM wamekuwa na uelewa Mkubwa kuhusu kuanzisha vikundi kwa ajili ya kupewa mikopo kama kusudio la Serikali hivyo kutotoa Mikopo kwa Halmashauri ni kukiuka maelekezo ya ilani ya Uchaguzi hivyo jambo hilo linaibua hisia za malalamiko kwa Vijana wengi nchini.

Katika mahojiano na waandishi wa Habari Mara baada ya kumalizika Ziara ya kikazi katika Mikoa hiyo Shaka Alisema kuwa kutoa mikopo kwa Vijana sio ombi Bali ni maelekezo yaliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wakati wa kampeni katika ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020.

Alibainisha kuwa Vijana wengi nchini wanamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika uwajibikaji wake hivyo ni lazima wasaidizi wa Rais katika ngazi ya Halmashauri kuongeza kasi ya utendaji na kuacha ubabaishaji wanaoendelea nao.

Katika Ziara hiyo Shaka amebaini udanganyifu Mkubwa uliofanywa na baadhi ya wagombea kwa kuwa na umri Mkubwa kuliko maelekezo ya umri unaotakiwa kikanuni ambapo ni miaka 30 pekee.

*KUHUSU ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA*

Shaka Alisema kuwa UVCCM inaheshimu sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa na Serikali inayoongozwa na CCM hivyo mikutano inayofanyika yote inaofanywa ndani kama ambavyo maagizo ya Serikali yameelekeza, hivyo wale wanaosema kuwa CCM inafanya mikutano ya nje ni wapotoshaji wakubwa waliokosa ajenda za kujadili.

Alisema kuwa Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu vyama vyote vilivyoshiriki  vilinadi ilani za vyama vyao lakini CCM ndio Chama kilichopewa dhamana na wananchi hivyo Chama na Jumuiya zake ni lazima kuzuru katika maeneo Mbalimbali nchini ili kujionea kiasi utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi unavyofanywa na watendaji wa Serikali.

Alisema kila unapofanyika uchaguzi na kupatikana Viongozi wawakilishi huwa inamalizika awamu ya kwanza ya kufanya siasa za jukwaani zenye kejeli na vitimbwi vingi hivyo jambo linalofuata ni kufanya siasa za kujenga nchi kwa kuwapatia maendeleo wananchi.

"Sisi na wenzetu tumetofautiana sana sisi kila tunapofanya mikutano kwa mujibu wa taratibu wenzetu wanapiga kelele utadhani wametekenywa mahala pakustua, ni lazima watambue kuwa CCM kuna Rasilimali watu, Rasilimali Kazi na tuna mipango na uratibu vitu ambavyo wenzetu wapiga kelele hawana"

"Wamekuwa wakitengeneza Propaganda ili kuwahadaa watanzania kwamba CCM inafanya maandamano jambo ambalo sio kweli na halina uhalisia kabisa hivyo tunawaomba watanzania kuwapuuza watu hawa" Alisisitiza Shaka Wakati wa mahojiano hayo

Ziara ya Naibu Katibu Mkuu UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka imeimarisha kwa kiasi kikubwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya zake ambapo Wananchi wamepata fursa ya kupata ufafanuzi wa mambo yaliyokuwa yakiwatatiza huku akiahidi kuendelea na Ziara katika maeneo Mbalimbali nchini hivi karibuni.

MWISHO

No comments:

Post a Comment