Monday, July 31, 2017

Rais wa Urusi, Vladimir Putin Kawafukuza wanadiplomasia 755 wa Marekani

Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameagiza kuondolewa wanadiplomasia na wafanyakazi 755 wa Marekani waliopo nchini humo na anafikiria kuchukua hatua za nyongeza kulipiza kisasi kwa vikwazo vya uchumi ilivyowekewa nchini hiyo.

Putin alisema jana katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa kwamba aliagiza hatua hizo kwa sababu “alifikiri ulikuwa wakati wa kuonyesha kwamba hawawezi kubaki bila kujibu mapigo."

Utekelezwaji wa agizo la usitishwaji shughuli za wafanyakazi hao wa ubalozi wa Marekani nchini Urusi unatarajiwa kuwa Septemba Mosi mwaka huu. Watabaki wafanyakazi 455.

Desemba 2016, aliyekuwa rais wa Marekani, Barack Obama aliamuru kutimuliwa wanadiplomaisa 35 wa Urusi kutokana na tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani kupitia njia ya mtandao.

Jumanne iliyopita mabunge yote mawili ya Congress ya Marekani yaliidhinisha kwa wingi wa kura vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi.

Mashirika ya ujasusi nchini Marekani yanaamini kuwa Urusi ilijaribu kuingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 kwa lengo la kumsaidia Donald Trump kupata ushindi.

Urusi imekuwa ikikanusha kuingilia kwa vyovyote uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment