Vikosi
maalumu vya majeshi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) vimepiga kambi kwenye eneo la mapango ya Amboni, Tanga kwa ajili
ya mazoez ya kijeshi.
Katika
mapango hayo, mwaka jana yalitokea mauaji yaliyofanywa na watu
wasiojulikana na kuzua hofu kwa wakazi wa eneo hilo ambao mwishowe
walihamishwa na Serikali.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkuu wa mpango huo, Meja Jenerali
Harrison Msebo, alisema vikosi hivyo vitakuwa vikifanya mazoezi katika
eneo hilo kama sehemu ya kupambana na ugaidi na uharamia baharini.
Kwa
mujibu wa Meja Jenerali Msebo, mazoezi hayo yajulikanayo kwa jina la EX
Matumbawe, yanatarajia kuanza Agosti 2 hadi Septemba mosi mwaka huu.
“Mazoezi
hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza Tanzania baada ya vikosi vya
majeshi ya nchi washirika kuanza kufanya mazoezi ya pamoja kwa ajili ya
kujihami dhidi ya matukio mbalimbali ya uhalifu tangu mwaka 2015.
“Pamoja
na mambo mengine, lengo letu ni kuhakikisha vikosi vya majeshi katika
nchi washirika vinajengewa uwezo wa kupanga na kutekeleza operesheni za
vikosi maalumu na kujifunza mbinu na weledi katika kupambana na matukio
ya uvamizi yanayoweza kufanywa na maharamia na magaidi.
“Mazoezi hayo yanatokana na mbinu za kupigana vita pamoja na matishio ya ugaidi kubadilika mara kwa mara.
“Hivyo kupitia mazoezi hayo, tutaweza kuvitayarisha vikosi vyetu dhidi ya mapambano ya aina yoyote yanayoweza kutokea,” alisema Meja Jenerali Msebo.
Alizitaja
nchi zenye majeshi yatakayoshiriki mazoezi hayo kuwa ni Afrika Kusini,
Botswana, Lesotho, Malawi, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema mazoezi hayo
yataimarisha uhusiano wa kijeshi baina ya nchi wanachama wa SADC na
yatawasaidia wanajeshi hao kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi
wao.
“Kwa
hiyo napenda kuwaomba wananchi, kwamba watoe ushirikiano wakati wote wa
mazoezi hayo ingawa pia nawaomba wananchi wasipende kuokota vitu
ambavyo wana hofu navyo.
“Kama
wananchi wakiona kitu wasichokielewa, basi watoe taarifa wahusika waje
kuvitambua badala ya kuviokota kwa ajili ya matumizi yao,” alisema Shigela.
Wakati
mazoezi hayo yakitarajia kuanza mwaka jana hali ilikuwa tete na ilizua
taharuki jijini Tanga baada ya watu wasiojulikana, kuua idadi kadhaa ya
watu katika eneo la mapango hayo.
Serikali
ililazimika kupeleka vikosi vya Jeshi la Polisi na askari wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kukabiliana na wahalifu hao.
Wakati
vikosi hivyo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi, vilikuwa vikiendesha
operesheni maalumu ya upekuzi ndani ya mapango hayo kwa lengo la
kukabiliana na wahalifu hao.
Kutokana na hali ya usalama kuwa tete katika eneo hilo, baadhi ya watu walilazimika kuhama makazi yao kuokoa maisha yao.
No comments:
Post a Comment