Monday, July 31, 2017

Kampeni ya ‘MAGUFULI BAKI’ Kuanza Nchi Nzima Hivi Karibuni

Kampeni ya ‘MAGUFULI BAKI’ iliyoanzishwa karibuni na mwanaharakati ambaye pia aliwahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015, Laurence Mabawa, inatarajiwa kuanza karibuni.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana , Mabawa alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kupigania rasilimali za wananchi wanyonge na masikini na kuunga mkono juhudi anazozifanya na hivyo kampeni hiyo inahamasisha yeye kubaki katika msimamo wake pasipo kusikiliza maneno ya watu.

“Napinga kwa nguvu zote, kama nilivyokwisha kufafanua toka mwanzo ,kampeni ya ‘Magufuli Baki’ ina lengo la kumtia moyo Rais Magufuli na kumwomba abaki katika msimamo wake wa kutetea maskini, wanyonge na kupigania rasilimali za taifa letu,

“Nirudie tena wito wangu kwamba nitazunguka nchi nzima kwa gharama zangu kupata fursa ya kuwasikiliza wananchi kupitia kampeni yangu inayojulikana kwa ‘Magufuli Baki’ kuhakikisha wananchi wanatoa maoni yao juu ya rais kuendeleza msimamo wake wa kiutendaji na sitavunjwa na propaganda za baadhi ya vikundi vinavyonikejeli mitandaoni pasipo kuthamini maendeleo anayoyafanya,” alisema.

Aidha alieleza kwamba toka aitangaze kampeni yake kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wanasiasa na wananchi ambao hutoa lugha za maudhi na kejeli kwa baadhi ya Watanzania wanaojitokeza hadharani kumpongeza Rais Magufuli na serikali yake.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 kifungu kidogo cha (1) na (2) kinatupa haki na fursa ya kutoa maoni na kueleza fikra zetu, hivyo amewaomba wanasiasa wasitumie kifungu hicho cha katiba kukivunja kwa kutoa maoni yenye kuudhi na kejeli, kwa hiyo, alisema, kitendo cha kushambuliana kwa maneno makali ni kosa kisheria.

Alisema kampeni aliyoianzisha itaweza kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao ambayo yatasambazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kuanzia mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment