Tuesday, June 27, 2017

Shein atahadharisha madereva kuepuka ajali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametoa mwito kwa madereva kutoendesha vyombo vyao kwa mwendo wa kasi, ili kuepuka ajali zisizo za lazima hasa katika kipindi hichi cha Sikukuu ya Idd el Fitr ambacho wananchi wengi hutumia huduma za usafiri wa barabarani wakiwemo watoto.

Dk Shein aliyasema hayo wakati akifanya mahojiano na watoto wanaotayarisha kipindi cha “Watoto na Sikukuu” kutoka Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Ikulu mjini Zanzibar, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za Sikukuu ya Idd el Fitr.

Alisema uendeshaji wa vyombo vya moto kwa kasi ni hatari, hali inayosababisha ajali zisizo za lazima. Aliwataka askari wa usalama barabarani kuwa makini dhidi ya madereva wote wanaoendesha kwa mwendo wa kasi.

Dk Shein aliwahimiza madereva kusherehekea sikukuu zote kwa kuendesha kistaarabu na kwa umakini huku wakizingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepuka sikukuu kugeuka kuwa majonzi.

“Nanyi watoto msije kuingia kwenye gari halafu mkawapampu madereva kwa kuwapigia kelele, ili waendeshe gari zao mbio, huku mkisema ndio babu, hivyo hivyo ongeza mwendo, si vizuri na mkiiona gari inakwenda mbio basi msipande,” alisisitiza Dk Shein.

Michezo shuleni

Alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha michezo kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuutekeleza Mpango wa ‘Sport 55’, unaolenga kuongeza hamasa ya ushiriki wa wanafunzi katika michezo kwa kuzipatia vifaa vya michezo shule 55 Unguja na Pemba kwa hatua ya awali, kutengeneza viwanja, mafunzo ya kiufundi na kiutawala kwa walimu na viongozi wa michezo kwa kila Wilaya na Mikoa.

Katika kutekeleza hilo, alisema tayari Sh milioni 300 zimeshakusanywa ili kutekeleza azma hiyo ya Serikali. Alisisitiza kuwa kila wilaya kutajengwa viwanja vya michezo na zitaanza wilaya tano na tayari viwanja viwili vimeshaanza kujengwa. “Tunafanya Mpango mkubwa ili watoto wapate kucheza na wacheze katika mazingira yalio bora na yalio mazuri.”

Dawa za kulevya

Kuhusu vita dhidi ya dawa za kulenya, Dk Shein alieleza mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupambana na dawa hizo kwa wanaoingiza, wanaouza na hata wale wanaotumia na hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Alitoa mwito kwa watoto kutoiga tabia za matumizi ya dawa za kulevya.

CREDIT: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment