Tuesday, June 27, 2017

January aishauri Bakwata kuunganisha vijana wasomi

 Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira ) Januari Makamba

MBUNGE wa Bumbuli, January Makamba amelishauri Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata), kuwaunganisha vijana wote wasomi wa Kiislamu.

Alisema vijana hao ni waliopo katika taasisi za serikali na binafsi ili waweze kushiriki katika mambo mbalimbali yatakayowezesha baraza hilo kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia ya sayansi na teknolojia.

Akizungumza juzi kwenye Baraza la Idd el Fitri, Makamba aliyetoa ujumbe kwa pande mbili kijana wa Kiislamu mwenyeji wa Tanga na kiongozi wa serikali, alisema kuwa baraza hilo limekuwa na changamoto kubwa ya kushindwa kuwaunganisha vijana wasomi waliopo katika maeneo mbalimbali nchini watakaosaidia kuliingiza baraza hilo na mabadiliko yaliopo duniani.

“Ndugu zangu viongozi wa Bakwata, taasisi yetu ina changamoto kubwa ya kutowaunganisha vijana wasomi waliopo katika maeneo mbalimbali ili muwahamasishe juu ya suala la dini na jumuiya hiyo... Tunataka baraza liimarike na liwe na hadhi kubwa kutokana na ukongwe wake katika mabadiliko yaliyopo hapa duniani,” alisema Makamba.

Mbunge huyo ambaye ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, alisema kuwepo kwa utaratibu huo wa kuwaunganisha vijana kutasaidia pia kuondoa umomonyoko wa maadili kwa vijana ambao hivi sasa wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kuzingatia mafundisho ya dini.

“Upo mmomonyoko mkubwa kwa vijana wa Kiislamu na ndio maana mara baada ya mfungo wa Ramadhani kwisha maeneo ya starehe hujaa vijana wetu wa Kiislamu...Ni lazima tutazame mfumo wetu wapi tumekosea ili vijana wetu waendelee kutii amri za dini,” alisema.

Makamba alisema lazima vijana wasome na wachukue mafunzo ya dini yao ili waweze kuja kurithi na mashehe pamoja na maimamu na kazi nyingine za Kiislamu ikiwemo kuwaunganisha katika kazi zote zinazoleta umoja miongoni mwa Waislamu na wasio Waislamu.

No comments:

Post a Comment