Rais
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi hataweza kutetea
nafasi yake hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Agosti 12
mjini Dodoma.
Hiyo inatokana na kushindwa kufika kwenye usaili ulioanza jana na kumalizika kesho kwa kuwa yupo rumande akikabiliwa na kesi.
Mbali
ya Malinzi, pia Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
aliyekuwa akiwania nafasi ya Makamu wa Rais TFF, pia amepoteza nafasi
hiyo kwa kuwa naye yupo rumande.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Revocatus Kuuli alisema mgombea ambaye
atakosa kufika kwenye usaili katika muda huo atakuwa amejiondoa kwenye
uchaguzi.
Malinzi,
ambaye aliingia madarakani mwaka 2013 alikuwa akitetea kiti chake
ambacho kingemfanya kuwa madarakani kwa miaka mingine minne iwapo
angechaguliwa.
Jana,
Malinzi (57), Katibu Mkuu wake, Mwesigwa Celestine (46) na Mhasibu,
Nsiande Mwanga (27) walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwamo ya kughushi na
kutakatisha fedha dola za Marekani 375,418 (Sh840 milioni).
Malinzi anashtakiwa kwa makosa 28, huku wenzake wakishtakiwa kwa makosa yasiyozidi manne.
Walisomewa
mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga ambaye alidai kuwa
katika shtaka la kwanza, Malinzi na Mwesigwa, Juni 5, 2016 wakiwa Dar es
Salaam kwa nia ya kudanganya, walighushi nyaraka zinazoitwa Maazimio ya
Kamati ya Utendaji (Executive Committee Resolution) wakionyesha Kamati
ya Utendaji ya TFF imebadili mtia saini wa akaunti ya benki ya TFF,
Edgar Leonard Masoud kuwa Nsiande Isawafo Mwanga wakati wakijua si
kweli.
Katika
shtaka la pili, Wakili Katuga alidai kuwa Septemba Mosi, 2016 katika
benki ya Stanbic, tawi la Kinondoni, Mwesigwa aliwasilisha nyaraka hiyo
ya kughushi.
Katika
shtaka la tatu, inadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi za TFF,
Malinzi alighushi risiti namba 308 ya Novemba 6, 2013 akionyesha
ameikopesha TFF dola za Marekani 9,300 (Sh19 milioni) wakati akijua si
kweli.
Katika
shtaka la nne, Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi ya
TFF, alighushi risiti namba 322 akionyesha ameikopesha TFF dola za
Marekani 10,000 (Sh20 milioni) wakati si kweli.
Shtaka
la tano, Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi ya TFF
alighushi risiti namba 323 akionyesha ameikopesha TFF dola za Marekani
18,000 (Sh37 milioni).
Katuga
alidai kuwa katika shtaka la sita, Desemba 17, 2013, Malinzi kwenye
ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 324 akionyesha ameikopesha TFF
dola 5,000 (Sh10 milioni).
Katika
shtaka la saba, Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, 2013 katika ofisi ya
TFF alighushi risiti namba 325 akionyesha ameikopesha TFF dola 1,032
(Sh2 milioni) wakati akijua si kweli.
Katika
shtaka la nane, Katuga alidai kuwa Machi 26, 2014, Malinzi alighushi
risiti namba 1956 akionyesha ameikopesha TFF dola za 40,000 (Sh84
milioni).
Wakili
huyo wa Serikali alidai katika shtaka la tisa kuwa, Machi 13, 2014,
Malinzi alighushi risiti namba 1957 akionyesha ameikopesha TFF dola
5,000 (Sh 10 milioni).
Aliendelea
kudai kuwa katika shtaka la 10, Mei 13, 2014, Malinzi alighushi risiti
namba 1624 akionyesha ameikopesha TFF dola 40,000 (Sh84 milioni).
Katika
shtaka la 11, Katuga alidai kuwa Mei 16, 2014, Malinzi alighushi risiti
namba 1634 akionyesha ameikopesha TFF dola 10,000 (Sh20 milioni).
Shtaka
la 12, Malinzi anadaiwa kuwa Julai 11, 2014, alighushi risiti namba
1860 akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola 15,000 (Sh30 milioni).
Katika
shtaka la 13, Malinzi anadaiwa kuwa Julai 11, 2014 alighushi risiti
namba 1861 akionyesha ameikopesha TFF dola 3,000 (Sh6 milioni).
Katika
shtaka la 14, inadaiwa kuwa Julai 15, 2014, Malinzi alighushi risiti
namba 1863 akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola 14,000 (Sh28 milioni).
Iliendelea
kudaiwa katika shtaka la 15 kuwa, Julai 15, 2014, Malinzi alighushi
risiti namba 1866 akionyesha ameikopesha TFF dola 4,000 (Sh8 milioni).
Katuga
alidai katika shtaka la 16, Malinzi anadaiwa kuwa Julai 25, 2014 ,
alighushi risiti namba 1876 akionyesha ameikopesha TFF dola 1,000 (Sh2
milioni).
Katika
shtaka la 17, wakili huyo alidai kuwa Agosti 19, 2014, Malinzi
alighushi risiti namba 1890 akionyesha ameikopesha TFF dola 5,000 (Sh10
milioni).
Kwenye
shtaka la 18, Katuga alidai kuwa Oktoba 11, 2014, Malinzi alighushi
risiti namba 1568 akionyesha ameikopesha TFF dola 1,200 (Sh2.4 milioni)
wakati akijua si kweli.
Shtaka
la 19, Malinzi anadaiwa kuwa Agosti 17, 2015 alikula njama ya kughushi
risiti namba 1511 akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola 5,000 (Sh 10
milioni).
Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Leonard Swai akisoma shtaka la 20, alidai kuwa Julai 22, 2015, Malinzi
alighushi risiti namba 2981 akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola 2,000
(Sh4 milioni).
Swai
akisoma shtaka la 21, alidai kuwa Mei 9, 2016, Malinzi alighushi risiti
namba 832 akionyesha ameikopesha TFF dola 7,000 (Sh14 milioni) wakati
akijua si kweli.
Katika
shtaka la 22, Swai alidai kuwa Juni 16, 2016, Malinzi alighushi risiti
namba 931 akionyesha ameikopesha TFF dola 10,000 (Sh20 milioni).
Inadaiwa
katika shtaka la 23, kuwa Agosti 2, 2016, Malinzi alighushi risiti
namba 947 akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola 1,000 (Sh2 milioni).
Akiendelea
kusoma hati ya mashtaka, Swai alidai katika shtaka la 24 kuwa Septemba
19, 2016, Malinzi alighushi risiti namba 1029 akionyesha ameikopesha TFF
dola 1,000 (Sh 2 milioni).
Swai
katika shtaka la 25, alidai kuwa Septemba 22, 2016, Malinzi alikula
njama ya kughushi risiti namba 1071 akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola
15,000 (Sh30 milioni).
Kwenye
shtaka la 26, ilidaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016
washtakiwa Malinzi, Mwesigwa na Mwanga kwa pamoja, walitakatisha fedha
kiasi cha dola 375,418 huku wakijua fedha hizo ni zao la kughushi.
Katika
shtaka la 27, Swai alidai kuwa Malinzi na Mwesigwa katika kipindi hicho
cha Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016 katika benki ya Stanbic, tawi la
kati la Kinondoni walijipatia dola 375,418 wakati wakijua fedha hizo
zimetokana na kughushi.
Katika
shtaka la 28, Mwanga anadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19,
2016 katika ofisi ya TFF aliwasaidia Malinzi na Mwesigwa kujipatia dola
375,418 kutoka benki ya Stanbic huku akijua upatikanaji wake umetokana
na kughushi.
Baada
ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo yanayowakabili Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa aliiambia Mahakama kuwa
upelelezi bado haujakamilika.
Jopo
la mawakili wa utetezi likiongozwa na Jerome Msemwa na Aloyce Komba
liliiomba Mahakama iwapatie dhamana washtakiwa hao lakini Mutalemwa na
mawakili wenzake wa Serikali waandamizi, Christopher Msigwa na Pius
Hilla walipinga dhamana kwa washtakiwa hao kwa madai kuwa mashtaka ya
kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana.
Hakimu
Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo, aliiahirisha hadi Jumatatu
ijayo atakapotoa uamuzi kama washtakiwa hao watapata dhamana hivyo,
walipelekwa rumande.
No comments:
Post a Comment