TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UFAFANUZI WA TAARIFA ZILIZOANDIKWA NA
BAADHI YA MAGAZETI JUU YA MGOGORO WA TANZANIA NA MALAWI KWENYE ZIWA
NYASA
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki inapenda kufafanua na
kuweka sawa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Magazeti ya tarehe
07 Desemba, 2016 kuwa mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye
Ziwa Nyasa unakaribia kuiva na kwamba Mgogoro huo unatarajiwa kumalizwa
na washauri wa kimataifa.
Taarifa
hiyo haikuwa sahihi. Ukweli ni kuwa, mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania
na Malawi kwa sasa upo chini ya Jopo la Viongozi Wastaafu wa Afrika
wanaotokea kwenye nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC). Jopo hilo linaongozwa na Mhe. Joachim Chissano, Rais
Mstaafu wa Msumbiji akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa
Botswana na Mhe. Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini.
Aidha,
Jopo hili ambalo liliundwa na Umoja wa Afrika kupitia Jukwaa la
Viongozi Wastaafu wa Afrika (Forum for Former African Heads of State and
Government) kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro huu, linaendelea na kazi
hiyo kwa kupitia taarifa mbalimbali na maandiko yaliyowasilishwa kwao na
Tanzania na Malawi. Vile vile, Jopo lilikwisha zikutanisha pande zote
mbili katika mashauriano ya awali yaliyofanyika nchini Msumbiji
Wizara
inapenda kuujulisha umma kuwa licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa
Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, mahusiano ya nchi hizi mbili
yamezidi kuimarika siku hadi siku katika Nyanja zote za kiuchumi,
kisiasa na kijamii. Hata wananchi wa pande zote mbili za Ziwa
wameendelea kuishi kwa amani na ushirikiano wa karibu.
Aidha,
katika kuimarisha uhusiano huu, Tanzania na Malawi zinatarajia kuwa na
mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano mapema mwakani. Mkutano huu
utawaleta watalaam wa nchi hizi mbili kutoka Sekta mbalimbali kwa lengo
la kujadili changamoto za ushirikiano katika sekta hizo, kubaini maeneo
mapya ya ushirikiano pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza miradi ya
pamoja itakayokubaliwa baina ya pande hizi mbili.
Pamoja
na mambo mengine, Mkutano huo unatarajiwa kujadili masuala ya
ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, usafirishaji, fedha,
nishati, utalii, ulinzi na usalama uhamiaji, uvuvi na ardhi.
Hivyo,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawaomba
Waandishi wa Habari, Wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla
inapohitajika kupata taarifa sahihi za suala hili kwenda kwenye Mamlaka
husika na kuziandika kwa usahihi kwa ustawi wa nchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Desemba, 2016.
No comments:
Post a Comment