Tuesday, December 27, 2016

Ridhiwani Kikwete, Joseph Haule Walaani Mkulima Kuchomwa Mkuki Mdomoni na Wafugaji

Wabunge  wa Mikumi, Joseph Haule na Chalinze, Ridhiwan Kikwete wamelaani kitendo kilichofanywa na jamii ya wafugaji kwa kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi kwa mkuki mkulima Augustine Mtitu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, kuhusu tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Upangwani, Masanze, Mikumi, wabunge hao waliezea kusikitishwa kwao na kutaka hatua zichukuliwe.

“Ni kitendo cha kusikitisha sana kwa hawa ndugu zetu wafugaji walijiamulia kufanya kitendo cha kinyama kama hiki, huu si ubinadamu kabisa,” alisema Haule.

Alisema mkulima huyo alichomwa mkuki na wafugaji wa Kimasai alipokuwa akimsaidia jirani yake kufukuza ng’ombe wasiharibu mazao shambani mwake.

Alisema Mwenyekiti wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji nao walijeruhiwa na wafugaji hao. “Sisi Ofisi ya Mbunge wa Mikumi tunatoa mwito kwa Serikali kubaini waliofanya vitendo hivyo na kuwakamata ili kuvikomesha,” alisema Haule.

Alisema atashirikiana na Serikali kukomesha migogoro isiyokwisha kati ya wakulima na wafugaji Kilosa.

Ridhiwan naye alilaani vitendo hivyo na kuishauri Serikali kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hilo.

“Ni lazima Serikali ije na majibu sahihi, ili kunusuru vita vya wenyewe kwa wenyewe visitokee kati ya jamii hizo. Si ajabu kusikia mtu kavunjwa mgongo, mwingine mlemavu, leo kapigwa mkuki wa midomo ukatokea shingoni, kilio hiki kipo katika masikio ya watu wengi kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji,” alisema.

Aliongeza: “Serikali isikie hili na kuchukua hatua stahiki ya kudhibiti kabla damu ya Watanzania wanyonge wanaotegemea kilimo kama kiinua mgongo chao hawajapotea. Kuna sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi, zitumike.”

Ridhiwan alisema jambo la msingi ambalo Serikali inatakiwa kujua ni kwamba hali ilivyo sasa, si ya kufanyia mzaha na waziri husika ayafanyie kazi.

Alisema binafsi analaani vitendo hivyo na kuiasa Serikali kujipanga vizuri kabla mambo hayajaharibika. “Yalianza Kilosa, Mvomero, Chalinze, Handeni, Kiteto na sasa Mikumi. Serikali jipangeni, kabla hapajachafuka,” alihadharisha.

No comments:

Post a Comment