Monday, October 17, 2016

'Walioiba' makontena waanza kujisalimisha

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema tayari baadhi ya watu waliotorosha makontena bandarini bila kukaguliwa, wameitikia agizo lake la kuwataka kujisalimisha na kufanyika ukaguzi ili kujiridhisha bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo.

Mwishoni mwa wiki, Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara ambao wanadaiwa kutorosha makontena 100 bandarini, wajisalimishe Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili yakaguliwe. Ili kutekeleza agizo hilo waziri huyo aliweka dawati la dharura kutoa huduma hiyo katika siku za mapumziko.

Alisema wafanyabiashara ambao wangekaidi agizo hilo, wangechukuliwa hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya asilimia 15. Ukaguzi huo ulitakiwa kufanywa na TBS kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (FCC). Lengo la ukaguzi huo ni kubaini bidhaa zilizoingizwa nchini na ubora wake.

Alisema kuna wafanyabiashara wanaleta makontena yana nguo, ambazo zina kiwango cha chini na wengine hawalipi kodi, wengine wanaleta vilainishi vya magari wakati hapa nchini, pia kuna kiwanda cha kuzalisha vilainishi hivyo, hivyo kuruhusu makontena kupita bila kukaguliwa ni kuua viwanda vya ndani.

Aidha, alisema anaipenda sana kazi yake ya uwaziri, ndio maana analazimika kufanya kazi za chini, ambazo zingefanywa na ofisa wa kawaida wa Shirika la Viwango (TBS).

Akizungumza jana wakati wa kuzindua Sensa ya Uzalishaji Viwandani ya Mwaka 2013, Mwijage alisema ili asiondolewe kwenye wadhifa huo na aliyemteua (Rais John Magufuli), ni lazima afanye kazi hata ya kukagua makontena kwani anafanya hivyo kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani.

“Aliyenipa kazi hii tajiri namba moja, ameniagiza nifanye hivyo, ndio maana naenda hadi mitaani kukagua makontena kazi ambayo ingefanywa na ofisa wa kawaida wa TBS,” alisema Mwijage na kutamba kwamba kazi yake hiyo imezaa matunda.

Alisema licha ya kuwepo baadhi ya watu kumkebehi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hatua yake ya kwenda mitaani kukagua makontena, alisema hatishiki kwani yeye kazi yake ya kwanza kuifanya ilikuwa ni ya ukaguzi na hivyo anaifahamu vyema kazi hiyo.

“Nawaambia hivi nitaendelea kwenda kukagua makontena, niacheni nifanye kazi yangu, acheni kuniandika kwenye mitandao,” alisema Mwijage.

Aliongeza “Nilianza kazi nikiwa navaa khaki wakati nafanya kazi hiyo ya ukaguzi, licha ya kuwa leo hii mimi ni waziri, ndio maana niliwaambia wafanyakazi wa TBS wasiwe na haraka ya kupanda vyeo, nani angejua mvaa kaki angepanda hadi kuwa waziri.”

Alisema kuna bidhaa zinatoka nje zikiwa hafifu na hazina ubora, zinaingizwa nchini na kubandikwa lebo ya bandia.

“Kwa mfano kuna tomato zinatoka nje hazina ubora, lakini wanaweka lebo ya bandia, sasa tusipokagua kontena hizi zinaonekana ni bidhaa za maana kuliko tomato za nyanya za Morogoro ambazo zina ubora wa asili.

“Natoa mwito kwa Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa nchini kwani zina ubora kuliko bidhaa zinazotoka nje. Tunataka waje na ukaguzi ufanyike kwa usahihi ili kujua ubora wao, na sisi tutaendelea kunadi tomato yetu ya hapa nchini na matokeo tukutane huko sokoni,” alisema.

Alisisitiza kuwa yeye pamoja na wizara yake wataendelea kufuatilia kila kontena linaloingizwa nchini ili kujua ubora wa bidhaa pamoja na ulipaji wa kodi.

Alisema hana nia mbaya na wafanyabiashara ila anachowataka ni kutaka wafanye biashara katika uwanja sawa wa kibiashara.

Pia alitoa mwito kwa wafanyabiashara kuhakikisha kwamba hawaleti nchini bidhaa, ambazo zinatengenezwa na viwanda ambavyo vimeajiri watu wengi nchini.

Alisema kuruhusu kuleta bidhaa hizo nchini ni kuua viwanda vya ndani na matokeo yake ndio kunazalishwa vijana wahalifu, kama wale wa kundi la Panya Road.

No comments:

Post a Comment