Friday, October 21, 2016

Vita ya Kukabili Njaa Yatangazwa......Mikoa Yote Yatakiwa Kuimarisha Mifumo ya Kuhifadhi Chakula


Mwezi mmoja tangu Serikali iseme usalama wa chakula ni kwa asilimia 123, jana Ofisi ya Waziri Mkuu imezitaka wizara, mikoa na halmashauri kuchukua hatua za kukabiliana na tishio la njaa ikiwamo kuzuia matumizi ya nafaka kutengeneza pombe. 
Pia, ofisi hiyo ya Waziri Mkuu imewataka wananchi kuhifadhi chakula baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kutabiri kuwa kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu, maeneo mengi ya nchi yatakuwa na mvua zitakazonyesha chini ya kiwango huku maeneo mengine yakikumbwa na ukame. 
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Mbaazi Msuya alisema hali hiyo itasababisha ukame na tishio la njaa katika baadhi ya maeneo ambayo hutegemea mvua katika kilimo. 
Msuya alisema kutokana na utabiri wa TMA, wananchi wanashauriwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahimili ukame. 
“Maofisa ugani wanatakiwa kutoa ushauri kwa wananchi kuhusu mazao wanayotakiwa kupanda kwenye maeneo yao,” alisema. 
Aliwataka wananchi kuweka akiba ya chakula cha kutosha hasa kwenye maeneo ambayo yanapata mvua chini ya kiwango. 
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Usalama wa Chakula wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, MaryStela Mtalo alisema idara hiyo itafanya kazi ya uratibu, ufuatiliaji na ukusanyaji na kutoa taarifa za chakula kwa wakati. 
 “Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula wanaelekezwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha ili kukabiliana na upungufu unaotarajiwa katika baadhi ya maeneo,” alisema. 
“Mikoa na Halmashauri zake zisimamie na kuimarisha mifumo ya kuhifadhi chakula baada ya mavuno ili kupunguza upotevu wa chakula na kuhakikisha chakula kinapatikana.” 
Taarifa hii ya tishio la njaa inapingana na ile iliyotolewa Septemba 8 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Tate Ole Nasha kwamba Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu hali ya chakula nchini kwa maelezo kuwa kuna ziada ya chakula zaidi ya asilimia 123 ikilichozalishwa msimu uliopita. 
Akizindua tovuti ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mjini Dodoma, Naibu Waziri Ole Nasha alisema hali ya chakula inaridhisha kutokana na ukweli kuwa uzalishaji wa chakula ni kwa asilimia 100 hali ya utoshelevu wa chakula ni asilimia 101 hadi 120 hali inayotafsiriwa kuwa kuna chakula cha kutosha kwa miaka mitatu hadi minne. 
“Nawasihi Watanzania kutunza chakula kilichopo ili kitumike sasa na baadaye, hali ya uwepo wa  chakula ndani ya nchi itaonyesha kuwa kuna usalama kwa wananchi na wanaweza kuendelea na  shughuli zao za kila siku,” alisema.
 Pia ni tofauti na taarifa iliyotolewa Jumanne iliyopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo Dk Florence Turuka kwamba wilaya 42 nchini zinakabiliwa na uhaba wa chakula huku Mkoa wa Kagera ukikumbwa na baa la njaa na ukame. 

Kutokana na ukame huo, ng’ombe waliokuwa wanauzwa kwa Sh 600,000 wilayani Karagwe sasa wanauzwa kwa Sh 20,000. 

“Licha ya kwamba ripoti ya dunia inaonyesha hali ya chakula duniani ni mbaya, Tanzania kipo chakula na kinatosheleza kwa kiwango cha juu cha asilimia 123,”alisema Turuka wakati akizindua ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa mwaka 2016 inayoonyesha kuwa dunia inakabiliwa na balaa la njaa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

No comments:

Post a Comment