Friday, October 14, 2016

TCRA Yapiga Marufuku Uuzwaji wa Samsung Galaxy note 7 Hapa Nchini


MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepiga marufuku uingizaji na usambazaji wa simu za mkononi za Smartphone Samsung Galaxy note 7 kwa kuwa zina matatizo ya betri.

TCRA pia imewataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua.

Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, amewataka watanzania wajihadhari kuitumia simu hiyo kwa kuwa Kampuni ya Samsung yenyewe imeiondoa sokoni.

“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri na mara mbili sasa imelipuka,” amesema Mungy.

Amewaomba watu wenye simu za aina hiyo kuzirudisha madukani haraka wabadilishiwe ama kurudishiwa fedha zao.

“Hata kama uliletewa zawadi kutoka nje ya nchi nawaomba warudishe huko   kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” amesema Mungy.

Hivi karibuni simu aina hiyo iliyothibitishwa na kampuni hiyo kuwa ilikuwa salama, ilishika moto kwenye ndege nchini Marekani.

Simu hiyo inadaiwa kushika moto ikiwa mikononi mwa abiria aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest Airlines.
 
Shirika hilo liliwaondoa kwa dharura abiria waliokuwa kwenye ndege  iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka Louisville, Kentucky, hadi Baltimore, Maryland muda mfupi kabla ya kupaa.

No comments:

Post a Comment