Kimbunga
kijulikanacho Matthew kimewaua takriban watu 900 nchini Haiti na
kusababisha maelfu ya wengine kupoteza makazi kabla ya kuvuma kuelekea
katika jimbo la Florida nchini Marekani siku ya Ijumma (07.10.2016).
Idadi ya
vifo nchini Haiti, taifa masikini zaidi katika bara la Amerika
iliongezeka hadi 887 huku taarifa zikianza kupokelewa kutoka vijiji na
maeneo ya mbali yasiyofikika kwa urahisi nchini humo ambayo yaliathirika
vibaya na kimbunga hicho.
Huku
mawasiliano ya simu yakiwa yamekatika, umeme kutokuwepo, barabara kujaa
maji, nyumba kuporomoka na madaraja kusombwa na mafuriko, msaada
umechukua muda kuwafikia walioathirika zaidi na kimbunga hicho kusini
magharibi mwa Haiti.
Chakula
kinaripotiwa kuwa haba katika taifa hilo ambalo bado linajaribu
kujikwamua kutokana na athari za tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba
mwaka 2010. Takriban watu saba wanaripotiwa kufariki kutokana na maradhi
ya kipindupindu, maambukizi yanayohofiwa yamesababishwa na maji ya mvua
kubwa kuchanganyika na maji taka.
Kimbunga Matthew chaitikisa Haiti
Vituo vya
afya vya vijijini vimefurukia wagonjwa miongoni mwao waliovunjika
mifupa na hawajapokea matibabu tangu siku ya Jumanne. Meli iliyobeba
makontena tisa ya chakula na dawa imeelekea katika eneo la Dame Marie.
Misaada
inayosafirishwa kwa njia ya barabara, majini na angani inapelekwa pia
katika maeneo mengine yaliyoathirika. Helikopta mbili za jeshi la
Marekani zimepeleka tani 50 ya maji, chakula na dawa katika eneo la
Grand'Anse. Ufaransa pia imetangaza inapeleka misaada Haiti.
Mashirika
ya kutoa misaada yamesema takriban watu milioni moja wanahitaji misaada
ya dharura nchini humo. Kulingana na Umoja wa Mataifa, katika baadhi ya
maeneo, asilimia 80 ya mimea imeharibiwa na kimbunga hicho.
Mamia ya
watu hawajulikani waliko na inahofiwa kuwa idadi ya waathiriwa huenda
ikaendelea kuongezeka huku shughuli za uokozi zikianza katika baadhi ya
maeneo ya pwani, siku nne baada ya kimbunga Matthew kuikumba nchi hiyo
ambayo imelazimika kuahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike siku ya
Jumapili.
Kimbunga
Matthew kinatajwa kuwa kibaya zaidi kuwahi kuikumba Haiti, nchi nyingine
za Carribean na Marekani katika kipindi kirefu.
Marekani katika hali ya tahadhari
Kimbunga
Matthew pia kilisababisha maelfu ya watu kuhamishwa makwao katika
majimbo ya Florida, Georgia, South Carolina na North Carolina nchini
Marekani ili kupeusha vifo na maafa. Rais wa Marekani Barack Obama
amewaomba watu wa majimbo hayo kuitikia wito wa kuhamia maeneo salama na
kuzingatia maagizo ya kiusalama. Obama aliwaambia wanahabari kuwa
uwezekano wa mafuriko, vifo na uharibifu mkubwa wa mali upo.
Kituo cha
Marekani kinachofuatilia vimbunga NHC, kimeshusha nguvu za kimbunga
hicho kilichaonza kuvuma siku ya Jummanne katika kiwango cha nne katika
vipimo vya Saffir Simpson ambapo kilivuma kwa kilomita 230 kwa saa, hadi
kiwango cha pili kufikia jana Ijumma kikivuma kwa kasi ya kilomita 195
kwa saa.
Kumeripotiwa
vifo vya watu wanne katika jimbo la Florida vinavyohusishwa na kimbunga
hicho lakini mpaka sasa hakujaripotiwa maafa makubwa katika miji ambayo
mafuriko yaliiangusha miti na kusababisha kiasi ya watu milioni moja
kukosa umeme.
Gavana wa
Florida, Rick Scott amewatayarisha wanajeshi wa ulinzi wa taifa 3,500
ili kusaidia hali kwenye jimbo hilo. Wataalam wanasema maeneo ya jimbo
hilo yatakuwa kwenye hali ya kudhibitiwa kwa wiki kadhaa baada ya
kimbunga hicho kupiga.DW
No comments:
Post a Comment