Saturday, October 8, 2016

Mambo muhimu ya kuzingatia unapokwenda kutoa hotuba ( 2)



Ndugu zangu,
Naomba nianze na tungo hii fupi...
" Sina sauti nzuri ya kuimba, siwezi kucheza muziki watu wakanistaajabia.
Najua siwezi kuchora. Najua siwezi kuandika kitabu kikapata tuzo.
Maneno yangu si ya kurembesha sana, yanatoka moyoni.
Kipaji nilichojaaliwa si kikubwa na wala si cha upekee duniani.
Lakini, wote waliojaaliwa vipaji si sharti wang'ae wakaonekana."
Jana tuliangalia sehemu ya kwanza ya maarifa haya http://mjengwablog.com/habari-za-kijamii/item/28117-mambo-muhimu-ya-kuzingatia-unapokwenda-kutoa-hotuba-1.html#.V_iQt_krLIU Basi, leo tuangalie mfano wa viongozi na hususan kwenye siasa na kwa kumwangalia mwanasiasa. Duniani hapa siasa inahusu sana sanaa ya mawasiliano. Kwa mwanasiasa, kama huiwezi sanaa ya kuwasiliana na wananchi, basi, ni sawa na mtu unayejiita fundi mekanika , lakini huwezi kushika spana.
Kwa baadhi yetu tuliopata bahati ya kusoma vitabuni na hata kuishi na kushuhudia kampeni za chaguzi mbali mbali za ndani na nje ya mipaka yetu, kuna mapungufu tunayoyaona. Mapungufu ambayo, yumkini wengine walio ndani ya siasa hawayaoni.
Hapa nitajikita kwenye eneo la mawasiliano ya mwanasiasa kwa wapiga kura. Kuna watakaokubaliana nami, kwamba kuwa mwanasiasa ni jambo moja, na kuwa na uwezo wa kuwasiliana na wapiga kura ni jambo jingine kabisa.
Wakati mwingine, bila wao wenyewe kujua, ukweli kuna wanasiasa wanaotumia fedha nyingi na kupata mavuno haba kwa makosa ya kiufundi kwenye kujipanga kwenye eneo hili la sanaa ya mawasiliano kwa umma.
Ni kawaida kushuhudia viongozi wenye ' kupotea' jukwaani bila kujua kuwa wameshapotea.
Na anayepotea jukwaani yawezekana akawa amenunua hata muda wa televisheni wa saa zaidi ya mbili na kwa gharama kubwa. Mathalan, kwenye kampeni za uchaguzi, anachoshindwa mwanasiasa ni kupata wa kumshauri vema namna ambavyo, angeweza kutumia dakika 45 tu za kuwa ' Live' kwenye runinga ambayo ingewaacha watu wengine wakipiga kuta kwa ngumi wakitamani uchaguzi uwe juma lijalo ili wamalize kazi.
Hiyo ndio sanaa ya mawasiliano. Imekuwepo tangu enzi za Wayunani, wakiita ' Retorik'. Kiongozi/ Mwanasiasa hutakiwi kuzungumza zaidi ya saa nzima.
Hapo kutakuwa na dalili zote za mhusika ' kujizamisha' mwenyewe kwenye bahari ya taarifa nyingi na zenye kumchanganya msikilizaji.
Msikilizaji hapaswi kumsikiliza mzungumzaji akafikia kufikiria mambo mengine nje ya yale yanayozungumzwa. Hivyo, kuna haja ya mzungumzaji mkuu kuwa na mbinu za kumbakisha msikilizaji wake kutoka sekunde ya kwanza mpaka anapomaliza kuzungumza.
Ni kwa namna gani?... Itaendelea kesho...
Maggid,
Iringa.

No comments:

Post a Comment