Monday, October 17, 2016

uni1
Katibu  wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa kimataifa wa Kamati Maalum ya NEC, CCM Zanzibar,  Hamad Yussuf Masauni akizungumza na viongozi wa Kamati ya siasa ya Wilaya ya Mjini kichama katika ofisi za Wilaya hiyo Makadara.
uni2
Katibu  wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa kimataifa wa Kamati Maalum ya NEC, CCM Zanzibar,  Hamad Yussuf Masauni, akikagua ujenzi wa Barabara ya ndani katika maeneo ya Boznia Kikwajuni Zanzibar.
uni3
Katibu  wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa kimataifa wa Kamati Maalum ya NEC, CCM Zanzibar,  Hamad Yussuf Masauni, uzinduzi wa mradi wa Maji safi na salama katika tawi la CCM Sebleni Mwembeboso jimbo la Kwahani Zanzibar.

Na Is-haka Omar,  Zanzibar

KATIBU wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa kimataifa wa Kamati Maalum ya NEC, CCM Zanzibar,  Hamad Yussuf Masauni amewataka wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali zote mbili ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ili ziweze kuwaletea maendeleo endelevu.

Kauli hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara ya kuimarisha uhai wa Chama katika Wilaya za Mjini na Amani kichama,  alisema endapo wananchi wataendelea kuziamini na kutoa ushirikiano wa dhati kwa serikali hizo maendeleo ya nchi yataimarika kwa haraka.  

Alieleza kuwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 unaofanywa na serikali katika maeneo mbali mbali nchini umetokana na sera pamoja na miongozo mizuri iliyowekwa na CCM.

Masauni Ambaye pia ni Mbunge wa tiketi ya CCM jimbo la Kikwajuni alieleza kuwa CCM ndio chama pekee chenye sera za kuwaunganisha wananchi wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla ili waishi kama watu wa taifa moja lenye uwezo na nguvu za kijamii na kiuchumi.

“CCM itaendelea kuwa imara endapo tutakuwa wamoja na wenye nia thabiti ya kulinda amani na utulivu wa nchi zetu.

Pia sote ni mashahidi juu ya juhudi zinazofanywa na serikali katika kuimarisha nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa lengo la kuhakikisha wananchi hasa wafuasi wa chama chetu  wanaishi katika maisha mazuri na yenye heshima yanayoendana na hadhi ya rasilimali tulizonazo”., alisema Masauni na kusisitiza kuwa maendeleo hayana itikadi za vyama , kabila na dini hivyo kila mtu anatakiwa kutoa ushirikiano kwa chama na serikali katika mipango ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Masauni ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi aliwataka vijana nchini kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani badala yake wakae pamoja na kubuni fursa za maendeleo zitakazowaingizia kipato.

Alieleza kwamba uchaguzi mkuu umekwisha na kilichobaki kwa sasa ni wananchi kuacha itikadi za kisiasa na kushirikiana kwa pamoja kujenga maendeleo ya nchi.

“Naomba Wananchi  tujenge utamaduni wa kufanya kazi za siasa wakati wa uchaguzi na ukimaliza tu basi sote mawazo na fikra zetu tuzielekeze katika harakati za ujenzi wa nchi yetu.,” alisisitiza Masauni.

 Akizungumza Katibu wa Wilaya ya Mjini Kichama, Fatma Shomari alisema kwamba hali ya kisiasa ndani ya wilaya hiyo imeendelea kuimarika toka kumalizika kwa Uchaguzi wa Marudio wa machi 20, mwaka huu.

Alieleza kwamba viongozi mbali mbali wa Chama na serikali hasa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani  wamekuwa wakiendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015/2020, kwa juhudi kubwa hali inayojenga matumaini kwa wananchi.

Katibu huyo alisema  Chama kinaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kuimarisha mji wa Zanzibar  ili uwe wa kisasa na unaoendana na hadhi ya nchi.

“Tunaomba wananchi waelewe kwamba serikali haina nia mbaya katika kutengeneza mji wetu lengo ni kuweka mji katika mazingira safi na yenye muonekano wa kisasa.” Alisema Fatma.

Akitoa taarifa fupi ya hali ya kisiasa ndani ya Wilaya ya Amani Kichama, Abdallah Mwinyi alisema wilaya hiyo ina jumla ya wanachama 25,998 ,wanawake 15,309 na wanaume 10,689.

Alisema katika juhudi za kuimarisha chama tokea mwaka 2012 hadi 2015 jumla ya wanachama 13,565 sawa na asilimia 52 wamelipa ada katika maeneo mbali mbali ya wilaya hiyo.

Mwinyi alieleza kwamba utekelezaji wa ilani ya CCM ndani ya wilaya hiyo umeendelea kwa kasi kubwa  ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji safi na salama pamoja na ukarabati wa barabara za ndani katika Majimbo ya Chumbuni, Magomeni na Shauri Moyo kwa lengo la kuwarahisishia wananchi huduma za kijamii.

Katika ziara hiyo, Masauni alitembelea na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo katika Wilaya ya Mjini ametembelea ujenzi wa Tawi la Mwembe Ladu na kuchangia kiasi cha shilingi 500,000 pamoja na mradi wa ujenzi wa uzio na mnara wa tanki la maji katika shule ya msingi Makadara.

Maeneo mengine ni uzinduzi wa mradi wa Maji safi na salama katika tawi la CCM Sebleni Mwembeboso uliogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni nane pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara za ndani katika maeneo ya Boznia hadi Maktaba Kuu Zanzibar iliyopo  Kikwajuni.

Kwa upande wa Wilaya ya Amani, ametembelea ujenzi wa barabara ya Ziwatuwe hadi Shauri Moyo pamoja na kuweka jiwe la msingi katika Tawi la CCM Shauri Moyo “B” na kuchangia kiasi cha shilingi 400,000.

Maeneo mengine yaliyotembelewa ni mtaa wa Mboriborini unaosadikiwa kufanyika vitendo vya uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya ambapo alitoa nasaha kwa vijana kuacha tabia za uhalifu badala yake watumie fursa zilizowazunguka kujiajiri wenyewe kupitia vikundi vya ujasiria mali.

No comments:

Post a Comment