Saturday, October 8, 2016

Bodi ya Mikopo (HESLB ) Yasitisha Mikopo Ya Walimu Wanafunzi Waliompiga Mwanafunzi Mbeya


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inautaarifu umma kuwa imesitisha mikopo ya elimu ya juu iliyokuwa ikitolewa kwa walimu-wanafunzi wanne waliosimamishwa masomo kwa kuhusika katika tukio la kumshambulia na kumuumiza mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya. Walimu hao walikuwa katika mafunzo ya vitendo.
1. Frank Msigwa - Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE)

2. John Deo- Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE)

3. Evance Sanga - Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE)

4. Sante Gwamaka - Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA)

Kwa utovu huo wa nidhamu, wanafunzi hao wamesimamishwa masomo na mamlaka husika kwa hiyo wamepoteza sifa za kuendelea kupokea mikopo. 
Mikataba inayosainiwa na wanufaika wa mikopo inawataka wanufaika kuzingatia masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na nidhamu na kufuata sheria na taratibu za vyuo na mamlaka halali.

Aidha, kwa mujibu wa taratibu za kukopeshwa, wanafunzi hawa watatakiwa kuanza kurejesha kiasi walichokopeshwa mara moja.

Bodi ya Mikopo inawakumbusha wanufaika wanaoendelea masomo kuzingatia masharti ya ukopeshwaji na kuheshimu sheria, kanuni taratibu na kuwa mfano mwema katika jamii. Mikopo na ruzuku zinazotolewa na Serikali ni kwa ajili ya kuwaandaa kuwa raia wema, waadilifu, na wachapa kazi ili kujenga uchumi imara na ustawi kwa wote.

Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
Mkurugenzi Mtendaji

Ijumaa, Oktoba 7, 2016

No comments:

Post a Comment