Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
akihutubia leo mkoani Dodoma katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya
wadadisi wapatao 187 watakaofanya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kuanza nchi nzima kuanzia wiki
ijayo. (Picha na Veronica Kazimoto)
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo ya
kina kuhusu Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania katika
hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo unaotarajia kufanyika nchi
nzima kuanzia wiki ijayo. (Picha na Veronica Kazimoto)
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard
Maboko akizungumza leo mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuhitimisha
mafunzo ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI
Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia wiki
ijayo. (Picha na Veronica Kazimoto)
Mratibu
wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 Bi.
Mariam Kitembe wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akimkabidhi Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kiasi cha
Shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000) zilizochangwa na wadadisi
wa Utafiti huo kwa ajili ya waathirika wa Tetemeko lililotokea mkoani
Kagera hivi karibuni. Mhe. Ummy Mwalimu amekabidhiwa fedha hizo wakati
wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo mkoani
Dodoma. (Picha na Veronica Kazimoto)
Baadhi ya
wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka
2016 wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani)
wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo
mkoani Dodoma. (Picha na Veronica Kazimoto)
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
(watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Ofisi ya Mtakwimu
Mkuu wa Serikali Zanzibar pamoja na wakufunzi wa Utafiti wa Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 mara baada ya kufunga mafunzo
ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 leo
mkoani Dodoma. (Picha na Veronica Kazimoto).
Na. Emanuel Ghula- Dodoma
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kutoa ruhusa kwa manesi
ambao ni wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania
wa mwaka 2016 ili kufanya utafiti huo.
Akizungumza
leo katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi hao iliyofanyika
mkoani Dodoma, Waziri Ummy amesema utafiti huu ni wa muhimu sana hivyo
Makatibu Tawala hawana budi kuwaruhusu manesi hao waliopata mafunzo
kufanya utafiti huo.
“Ninawaagiza
Makatibu Tawala wote nchini kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa manesi
mliopo hapa leo ili muweze kulisaidia taifa letu kwa kutuletea takwimu
sahihi zitakazosaidia katika kutunga sera na kupanga mipango ya
maendeleo hususani katika suala zima la afya”, ameagiza Mhe. Ummy
Mwalimu.
Amefafanua
kuwa, takwimu hizi zitasaidia kuboresha juhudi kubwa zinazofanywa na
Serikali za kusogeza huduma zinazohusiana na VVU kama vile huduma za
upimaji wa VVU bure katika vituo vya kutolea huduma za afya vya
Serikali, kutoa huduma ya kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto (PMTCT) pamoja na utoaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU
zijulikanazo kama ARV.
“Utafiti
huu ni wa kipekee ukilinganisha na tafiti zingine zilizofanywa
zinazohusu UKIMWI kutokana na kujumuisha upimaji wa homa ya ini ambao
umekuwa tishio katika baadhi ya nchi barani Afrika”, amesisitiza Mhe.
Ummy.
Aidha,
Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi wote nchini kutoa ushirikiano kwa
wadadisi watakaopita katika kaya mbalimbali zilizochanguliwa kwa ajili
ya kufanya utafiti huu.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina
Chuwa amesema utafiti huu utahusisha watu wote kwenye kaya zipatazo elfu
kumi na sita (16,000) zilizochaguliwa kitaalam na kuwafikia watu wazima
wapatao elfu arobaini (40,000) na watoto zaidi ya elfu nane (8,000).
Dkt.
Chuwa ameeleza kuwa, takwimu hizi zitaisaidia Serikali katika kupanga na
kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zinazohusu sekta ya afya
nchini hususani upatikanaji wa huduma za afya.
Wadadisi
wapatao 187 ambao ni manesi kutoka hospitali mbalimbali nchini,
wamemaliza mafunzo ya Utafiti wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI ambao
unatarajia kuanza wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment