Colombia
itapiga hatua kubwa kuelekea kuliepuka jinamizi la muda mrefu la
machafuko wakati serikali na kundi la waasi nchini humo watakaposaini
mkataba wa amani uliopatikana baada ya miaka minne migumu ya mazungumzo
Umuhimu
wa muafaka huo ni mkubwa mno: mgogoro wa Colombia uliodumu kwa zaidi ya
miongo mitano, kwa sehemu ukichochewa na biashara ya dawa za kulevya
aina ya cocaine, umeua zaidi ya watu 220,000 na kuwaacha wengine milioni
8 bila makaazi. Ili kuonyesha umuhimu wa siku hii, mkataba huo
utasainiwa na Rais wa Colombia Juan Manuel Santos na kamanda mkuu wa
Revolutionary Armed Forces of Colombia – FARC, mpiganaji muasi
anayefahamika kwa jina la utani la Timochenko. Akizungumza katika mkesha
wa siku hii, Rais Santos amesema "Nadhani juhudi zote zilikuwa muhimu
na sasa tunastahili kufanya juhudi kubwa zaidi ili kuufanikisha mkataba
huu kwa sababu hatuna kikwazo mbele yetu. Natumai kwa pamoja, sote, yani
wale wanaounga mkono kura ya "Ndiyo" na wale wenye wasiwasi..kuwa
tunaweza kuungana baada ya kura ya maoni kupita na tunaweza kuitengeneza
nchi mpya pamoja".
Marais 15
wa Amerika Kusini, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry wanatarajiwa kushuhudia
tukio hilo la kihistoria katika mji wa kikoloni wa Cartagena.
Zaidi ya
wageni 2,500 walioalikwa kwenye sherehe hiyo wametakiwa kuvalia nguo
nyeupe kama ishara ya amani, na Santos atautia saini mkataba huo wa
kurasa 297 kwa kutumia kalamu iliyotengenezwa na ganda lililotumika
vitani.
Kutiwa
saini mkataba huo hakutakuwa mwisho wa mambo hata hivyo. Wacolombia
wanapewa fursa ya kuwa na usemi wa mwisho wa kuidhinisha au kupinga
mkataba huo katika kura ya maoni ya Oktoba 2. Uchunguzi wa maoni
unaonyesha ushindi wa kura ya "ndiyo”, lakini baadhi ya wachambuzi
wanaonya kuwa idadi ndogo ya wapiga kura huenda ukawa habari mbaya kwa
changamoto nyingi zinazoikabili nchi hiyo katika utekelezaji wa muafaka
huo muhimu.
Miongoni
mwa hatua kubwa na zenye utata zaidi itakuwa ni kuzifungua kesi za
uhalifu wa kivita dhidi ya waasi na wahusika wa serikali. Chini ya
kanuni za mkataba huo, waasi watakaoweka chini silaha zao na kukiri
makosa yao watasamehewa kifungo cha jela na kutakiwa kuwafidia
waathiriwa kwa kufanya kazi ya maendeleo katika maeneo yaliyoathirika
pakubwa na mgogoro huo.
Serikali
pia imeahidi kushughulikia suala la ugawaji usiokuwa wa usawa wa
mashamba, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likizungumziwa na FARC tangu
kundi hilo lilipoanzishwa kama jeshi la wakulima wadogowadogo mwaka wa
1964, na serikali ilikubali kushirikiana na waasi ili kuwapa maendeleo
mbadala maelfu ya familia zinazotegemea biashara ya cocaine. Kama
mkataba huo utaidhinishwa na kura ya maoni, basi wapiganaji karibu 7,000
wa FARC wataanza kuhamishwa hadi maeneo 28 katika kipindi cha miezi
sita ijayo ambapo watasalimisha silaha zao kwa waangalizi
watakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
DW
No comments:
Post a Comment