Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kubadilisha vitambulisho
vyote vya zamani ambavyo havina saini, huku ikitarajia kutoa
vitambulisho vipya vyenye saini kwa wananchi wote, waliokamilisha
taratibu za usajili na utambuzi kwa kuchukuliwa alama za kibayolojia,
ikiwemo alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki.
Aidha, inatarajia kutoa vitambulisho vipya kuanzia Septemba 14, mwaka huu katika ofisi zote za Nida za wilaya.
Taarifa
iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew
Massawe, ilisema kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika
sambamba na vipya huku taratibu za kuvibadilisha zikiendelea.
‘’Kutokana
na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji
zilizomo ndani ya kifaa maalumi kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji;
ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumikakatika huduma
mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma,’’ alisema Massawe.
Alisema
kuwa ofisi za wilaya zilizoanza usajili wa vitambulisho hivyo vipya kwa
Tanzania Bara na Zanzibar ni mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi,
Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Ruvuma na Dodoma.
‘’Waombaji
wote ambao vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa
maandishi katika simu zao za mkononi kuwafahamisha kufika vituo vya
usajili kuchukua vitambulisho vyao,’’ alisisitiza Massawe.
Alifafanua
kuwa wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na
kuendelea na kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, wajitokeze
kwa wingi kusajiliwa ili kupata vitambulisho hivyo.
‘’Kwa
wale ambao walisajiliwa kupitia Daftari la Kudumu la Mpiga Kura la Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Nida iko mbioni kuanza kutoa nambari za
utambulisho wakati taratibu za uzalishaji zikiendelea,’’ alisema.
Pia
aliwakumbusha wananchi kutunza vitambulisho vyao ili kuepuka gharama
kwani kitambulisho cha awali kilitolewa bure na iwapo kitapotea, ili
kupata kingine lazima mtumiaji alipie.
Aliongeza
kuwa kwa sasa vitambulisho hivyo vimeanza kutumika katika baadhi ya
huduma hususani kwenye benki kwa ajili ya kufungua akaunti na
kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupata huduma.
No comments:
Post a Comment