Tuesday, September 13, 2016

Mrema Awapongeza Wabunge wa UKAWA Kwa Kukubali Kurudi Bungeni

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Taifa, Augustine Mrema amewapongeza wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa kuamua kuacha kususa kuhudhuria vikao vya Bunge kushinikiza Naibu Spika, Tulia Ackson ajiuzulu au aondolewe kwenye wadhifa huo.
Mgomo huo ulisababisha wabunge wa Ukawa kutoshiriki kwenye Bunge la Bajeti, jambo ambalo limesababisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ipitishwe bila wabunge wa upinzani kuijadili na kuchangia mawazo yao bungeni.

Kwa mujibu wa barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai, Mrema ameeleza athari ya mgomo huo wa Ukawa kuwa ni kusababisha bajeti ya serikali ipitishwe kwa mawazo ya upande mmoja wa chama tawala.

Aidha, ilieleza kwamba mawazo ya wananchi kutoka kwenye majimbo yanayoongozwa na wabunge wa Ukawa yalikosekana, hivyo kuwafanya wabunge hao kuwanyima haki wapiga kura wao, kwa kuwakosesha uwakilishi kwenye Bunge la Bajeti.

“Bunge la bajeti ni kikao nyeti kwa vile linajadili na kupitisha mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka husika, ambayo yanamhusu na kumgusa kila mwananchi, hivyo haikuwa busara kwa wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge la Bajeti na kuwafanya wapiga kura wao wakose uwakilishi kwenye kikao nyeti kama hicho,” alisema. 
Mrema alisema, kuwepo kwao bungeni kungeweza kusaidia kuboresha bajeti hiyo kutokana na michango yao ya mawazo ambayo wangeyatoa na kupata bajeti bora zaidi kwa manufaa ya taifa.

“Sisemi kwamba bajeti iliyopitishwa ni mbaya, lakini kuwepo kwa wabunge wa upinzani kungesaidia kuboresha ili iwe nzuri zaidi kwa manufaa ya wapigakura wao waliowachagua majimboni mwao,” alisema.

Alisema “Hata kama Naibu Spika alikuwa na kasoro katika utendaji wake wa kazi, lakini Ukawa hawakupaswa kususa vikao vya bunge hilo, badala yake wangetafuta ufumbuzi wa suala kwa kufuata njia za kikatiba na kisheria, ikiwemo kutumia kanuni za Bunge.”

Alisema kwa kususa vikao vya Bunge, Ukawa wamesababisha madhara makubwa kwa wananchi hususani wapigakura wao ambayo hawawezi kulipika na wanaweza wakawaadhibu kwa kosa hilo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, kwa sababu wananchi waliwachagua ili kwenda kuwawakilisha bungeni na si kwenda kususia vikao vya Bunge.

“Sisi TLP tunaona kwamba Ukawa wamedhoofisha upinzani badala ya kuimarisha upinzani kama wenyewe wanavyodai, kwani huwezi kuimarisha upinzani kwa kususia vikao vya Bunge hususani Bunge la Bajeti,” alisema.

Alisema Ukawa wanapaswa kujifunza kwamba kususa vikao si mwarobaini wa kutatua mgogoro ya kisiasa, bali migogoro ya kisiasa hutatuliwa kwa kupitia njia za vikao na mazungumzo. 
Hata hivyo, alisema madhara yaliyopatikana kutokana na mgomo huo hayawezi kulipika kwa sababu Bunge la Bajeti limeshapita na haliwezi kurudiwa.

No comments:

Post a Comment